"Sikuachwa, niliachia mimi!" Mamake Zuchu, Khadija Kopa afunguka kuhusu talaka zake nne

Muhtasari

•Kopa ambaye ni mama ya staa wa Bongo Zuhura Othman almaarufu kama Zuchu alisema kwamba amekuwa akiwatema waume zake baada ya kuhisi haridhishwi nao.

•Alisema kwamba kwa wakati mume wake wa kwanza alirudi tayari alikuwa ameposwa na mume wa pili.

•Kopa alisema kwamba baada ya kuondoka kwa ndoa ya pili aliolewa na mwanaume tapeli ambaye hakuwapenda watoto wake.

Khadija Kopa na Bintiye Zuchu
Khadija Kopa na Bintiye Zuchu
Image: HISANI

Gwiji wa Taarab kutoka Zanzibar Khadija Omar Kopa amekiri kuwa mpaka sasa amewahi kuwa kwenye ndoa nne tofauti.

Akiwa kwenye mahojiano na Wasafi Media, mtunzi huyo shupavu wa nyimbo aliweka wazi kuwa  mara zote zile yeye ndiye amekuwa akimtema mume, sio yeye kuachwa. 

Kopa ambaye ni mama ya staa wa Bongo Zuhura Othman almaarufu kama Zuchu alisema kwamba amekuwa akiwatema waume zake baada ya kuhisi haridhishwi nao.

"Kwa talaka zangu nne, sikuachwa nimeachia mimi. Ningewaambia, wewe mwanamume huridhishi kaa ngozi ya futi, ebu nenda. Sio eti sikuishi nao vizuri, nimeishi na waume zangu vizuri na bahati mbaya wanaondoka na wanapojutia na kutaka kurudi, mimi sina muda wao tena" Kopa alisema.

Kopa alifichua kwamba aliomba talaka yake ya kwanza baada ya  mume wake kumuacha akiwa mjamzito na kupotea kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili.

"Nilienda mahakama ya Kadhi kuelezea wakasema mwanamume akifikisha miaka miwili naweza nikapewa talaka, nikapewa. Nilitaka mimi mwenyewe. Kwa bahati mbaya nilipopewa talaka naye akarudi" Alisimulia Bi Kopa.

Alisema kwamba kwa wakati mume wake wa kwanza alirudi tayari alikuwa ameposwa na mume wa pili.

Kopa alisema kwamba mume wake wa pili alikuwa mwenye vurugu na alikuwa na mazoea ya kulala nje mara kwa mara.

Alidai kwamba aliamua kujiondoa kwenye ndoa hiyo kwa kuhofia maisha yake huku akifichua kwamba kwa wakati mmoja mumewe aliwahi kumburura chini akiwa mjamzito.

"Nilienda mahakamani kwetu Zanzibar nikamhadithia Shekhe. Shekhe alituma barua akaitwa. Alipofika aliuliza 'nimpe talaka ngapi?'. Nilimwambia anipe tatu. Shekhe aliniambia nichukue moja tu kwani huenda akarudi nimpe hizo zingine wakati huo" Alisema.

Kopa alisema kwamba baada ya kuondoka kwa ndoa ya pili aliolewa na mwanaume tapeli ambaye hakuwapenda watoto wake.

Alisema watoto wake wakiongozwa na marehemu Omari walimshinikiza agure ndoa hiyo baada ya mumewe kukamatiana visu na kifungua mimba wake.

"Nilikaa naye miaka mitano. Niliambia watoto wangu wawe na subira. Ningepigiwa simu na kuambiwa kwamba mume wangu ako mahali anakula vibanzi na mwanamke mwingine huku  akimfundisha kuendesha gari yangu" Alisema.

Mwanamuziki huyo alifichua kwamba wakati aliomba mumewe huyo wa tatu talaka aliiandika haraka ila akaanza kujuta siku tatu  baadae.

Kopa alisema kwamba mume wake wa mwisho, Jaffari Ally ambaye alifariki takriban miaka tisa iliyopita ndiye aliyekuwa mzuri kati ya wote.

Alieleza kwamba marehemu Ally aliwapenda watoto wake sana na vilevile wanawe walimpenda pia.

"Kwenye watu kumi mwanaume kama yule huwa mmoja, ukipata mwanaume kama huyo unafurahia. Nikawa nauliza Mungu 'Kwa nini mwanaume huyo hungenipa yeye akiwa wa kwanza, sasa tungekuwa tunasherehekea miaka kumi'" Alisema.

Kopa alisema amewahi kuolewa na mume mwenye wake watatu tayari na kueleza kwamba hakuwahi kuzozana na wake wenzake.

Alisema kwa sasa hana hamu ya ndoa kwa kuwa anahofia kupatana na mwanaume ambaye hataridhia kuwa naye. 

Hata hivyo alidai kwamba kunao wanaume wengi ambao wamekuwa wakimumezea mate wakitamani kumuoa.