"Ni mpole sana!" Kakake Vera Sidika azungumzia uhusiano wake na shemejiye Brown Mauzo

Muhtasari

•Josh alieleza kwamba Mauzo amekuwa akimsaidia sana katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuunga mkono taaluma yake changa ya muzik

•Alimtaja Brown Mauzo kama shemeji bora zaidi na kueleza kuwa yeye ni mtu mtulivu anayeelewana vizuri sana na watu.

Kinger Josh azungumzia uhusiano wake na Brown Mauzo
Kinger Josh azungumzia uhusiano wake na Brown Mauzo
Image: MPASHO

Mwanamuziki Joshua Mung'asia almaarufu kama Kinger Josh amefunguka kuhusu jinsi uhusiano wake na mume wa dada yake Vera Sidika, Brown Mauzo ulivyo.

Akiwa kwenye mahojiano na Mpasho, Josh alifichua kuwa kuna uhusiano mzuri kabisa kati yake na mwanamuziki huyo na kueleza kwamba amekuwa na ushawishi mkubwa sana katika maisha yake.

Kaka huyo mdogo wa Vera alieleza kwamba Mauzo amekuwa akimsaidia sana katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuunga mkono taaluma yake changa ya muziki.

"Brown Mauzo ni shemeji yangu. Tuko poa sana. Yeye ni mwenye kusaidia sana hasa kwa kuwa yeye ni mwanamuziki aliyebobea, ananioyesha njia bora za muziki. Huwa ananiambia cha kufanya na kile ambacho sifai kufanya. Yeye ana uzoefu kubwa. Kuwa naye imekuwa nzuri sana" Josh alisema.

Msaanii huyo chipukizi alifichua kuwa Mauzo alimsaidia sana katika kutengeneza wimbo wake wa kwanza 'Miss You' ambao alitoa hivi majuzi.

Josh alimtaja Brown Mauzo kama shemeji bora zaidi na kueleza kuwa yeye ni mtu mtulivu anayeelewana vizuri sana na watu.

"Yeye ni wa msaada sana, namshukuru sana. Yeye ni mtu mpole sana, hana drama nyingi, ana subira sana" Josh alisema.

Mwanamuziki huyo hata hivyo alisusia kueleza iwapo ni kweli dadake amefunga ndoa rasmi na Brown Mauzo.