Eric Omondi azungumzia madai ya kukana mwanawe na Jacque Maribe

Muhtasari

•Eric alisisitiza kuwa yuko kwenye harakati ya kutafuta mchumba ambaye watazaa naye watoto wawili wa kike.

•Eric alisema kuwa anatamani sana kuwa na familia yake huku akieleza kwamba kwa sasa nyumba yake sio kamili bila mke na watoto.

Eric Omondi na Jacque Maribe
Eric Omondi na Jacque Maribe
Image: HISANI

Mchekeshaji mashuhuri Eric Omondi amefafanua maana ya matamshi yake ya hivi majuzi kuwa hana mke na mtoto yeyote.

Hivi majuzi Omondi akiwa katika ziara ya kikazi nchini Tanzania alidai kuwa wakati wake wa kutafuta mke ambaye wataanza  familia pamoja naye umefika kwani hivi karibuni atakuwa anafikisha miaka 40.

"Natafuta mke. Nimekuwa nikitafuta mke kupitia Wife Material imeshindikana. Nahitimu miaka 40. Sina mtu, sina mtoto, sina bibi" Eric alisema.

Matamshi hayo yaliibua gumzo kubwa mitandaoni wengi wakidai kuwa yalimaanisha amemkana mtoto wa mtangazaji Jacque Maribe anayeaminika kuwa wake.

Akiwa kwenye mahojiano na Eve Mungai, Eric aliweka wazi kuwa alimaanisha kwamba kwa sasa hana mke wala watoto nyumbani.

Mchekeshaji huyo alisisitiza kuwa yuko kwenye harakati ya kutafuta mchumba ambaye watazaa naye watoto wawili wa kike.

"Kila mtu huelewa tofauti. Ujumbe wangu ulikuwa, nafikisha miaka 40  mnamo Machi 9 na  ukienda kwangu hakuna bibi. Pia hutapata watoto. Nataka hayo mwaka huu, nataka watoto wawili wa kike" Eric alisema.

Alisema kuwa anatamani kupata watoto wa kike kwa kuwa amelelewa katika familia ya wavulana wengi  na msichana mmoja pekee na angetaka utofauti.

Eric alisema kuwa anatamani sana kuwa na familia yake huku akieleza kwamba kwa sasa nyumba yake sio kamili bila mke na watoto.

"Nataka niwe na familia. Nilimaanisha ninapoelekea kufikisha miaka 40, nadhani ni wakati mwafaka wa kuenda kwa nyumba iliyo na mtoto na mke, mtu nimeoa" Eric alisema.

Mwishoni mwa mwaka jana mchekeshaji huyo na mzazi mwenzake Jacque Maribe walijibizana vikali mitandaoni kuhusiana na mtoto wao mwenye umri wa takriban miaka saba.