Hatimaye Mulamwah asema kiini cha kuvunjika kwa mahusiano na Sonie

Muhtasari

Mchekeshaji Kendrick Mulamwah amefungulia mwanga wa kile kilichofanya mahusiano yake na muigizaji Carrol Sonie yakavunjika.

• 'Alikuwa anataka tupige sherehe ya 8K na mimi ni mtu natoka katika sehemu ambayo pesa zinathaminiwa sana, kwa hiyo sikuwa nakubali', alisema Mulamwah

Image: INSTAGRAM// MULAMWAH

Mchekeshaji Kendrick Mulamwah amefungulia mwanga wa kile kilichofanya mahusiano yake na muigizaji Carrol Sonie yakavunjika.

Mulamwah kwa mara ya kwanza alifichua kwamba sababu kubwa ya kuvunja mahusiano yao ni kwa sababu mpenzi wake alikuwa anataka watumie pesa nyingi hali ya kuwa mchekeshaji huyo hakuwa anataka.

“Sisi tunajua pahali tumetoka, ni vizuri kutengeneza pahali tumetoka. Mimi kuishi hiyo nyumba ya 9K haimaanishi kwamba sina pesa, lakini ukiniambia tuende tupige sherehe mahali, twende tutumie elfu 8, wakati mimi najua kuna mtu nyumbani anatuchungia ng’ombe na analipwa elfu mbili, mimi nikifiria hizo elfu nane na elfu mbili haziendi Pamoja. Mimi natoka sehemu ambayo pesa zinathaminiwa sana, siwezi tumia pesa kiholela hivo. Sisi issue yetu ilitokea tu hapo whereby najaribu ku instill sense namwambia hatuko mitandaoni kuonesha vile tunakaa bali tuko pale kazi, lakini hakuwa ananisikia,” alisema Mulamwah.

Akizungumza na Dr. Ofweneke, Mulamwah alisema pia kwamba mahusiano hayo yalivunjika kwa mara ya pili kwa sababu ya makosa ya awali kujirudia mara kwa mara kutoka kwa mpenzi wake na ni yeye alitaka waachane kwa sababu alisema hawezi vumilia kuona makosa hayo ambayo alishayasamehe yanaendelea kujirudia.

“Kuna mambo mengi sana yaliyokuwa yakijirudia, kwa mfano mtu alikukosea na kitu fulani ama kwa mfano mtu akiuwa Rafiki yako kwa kutumia nyundo, na ukamsamehe, lakini tena kila mara mtu huyo anatembea na ile nyundo. Hapo sasa unamuona na ile nyundo na unakumbuka alichokifanya. Hicho ndicho pia kitu kilitokea kwa mahusiano yetu na kwa sababu mimi huwa nakumbuka nikiona kitu kilichotokea nyuma, niliona ni vizuri tusiende mbali sana, afadhali sai at the early stage itakuwa poa,” alisema Mulamwah.

Alipoulizwa kama huwa wanazungumza na aliyekuwa mpenzi wake na kama anaona mwanao, Mulamwah alisema kwamba Sonie hajamuwekea vikwazo vyovyote na kwamba huwa wanazungumza na kuelewana ni vipi na lini ataona mwanawe.

Vile vile mchekeshaji huyo alisisitiza kwamba mahusiano yao yalivunjika kitambo wakati ujauzito ulikuwa miezi mitatu pekee ila wakaelewana wakae Pamoja mpaka mtoto azaliwe.

Mchekeshaji huyo pia amesisitiza kwamba mtoto aliyezaliwa na Sonie ni wake na ndio maana anawajibika kama baba na hivyo kuyafutilia mbali madai yaliyozuka kwamba waliachana kwa sababu ya mtoto huyo.