Kabi Wajesus atangaza azma ya kuwania Useneti

Muhtasari

•Mwanavlogu huyo amedokeza kuwa ananuia kuwa katika Seneti lijalo ingawa hajaashiria kaunti ambayo anakusudia kuwakilisha.

Image: INSTAGRAM// KABI WAJESUS

Mwanavlogu Peter Kabi wa 'The Wajesus Family' amedokeza mpango wake kujitosa katika siasa na kuwania kiti cha useneti.

Katika ukurasa wake wa Instagram, Kabi amepakia picha akiwa ameng'aria suti maridadi na kuambatabisha na ujumbe unaoashiria kuwa huenda akawa debeni katika uchaguzi wa mwezi Agosti.

Mwanavlogu huyo amedokeza kuwa ananuia kuwa katika Seneti lijalo ingawa hajaashiria kaunti ambayo anakusudia kuwakilisha.

"Seneta Kabi Wajesus .. Bashiri kaunti?" Kabi aliandika chini ya picha hiyo.

Kabi ambaye ana ufuasi mkubwa kwenye mitandao ya kijamii alizaliwa na kulelewa katika mtaa wa Kayole, kaunti ya Nairobi.

Baadhi ya wanamitandao wamependekezea mwanavlogu huyo kuwania useneti wa aidha Murang'a, Kiambu ama Nyeri kwani anafahamika kuwa na asili ya jamii ya Kikuyu.

Iwapo kwa kweli Kabi anakusudia kuingia siasani basi atakuwa anajiunga na orodha kubwa ya wasanii ambao wamejitosa siasani mwaka huu. Baadhi yao ni Jalang'o, Prezzo, MC Jessy, Jamal Gaddafi, Njogu Wa Njoroge na wengineo.