Milly Chebby afunguka kuhusu kuharibika kwa mimba yake

Muhtasari

•Alisema alikuwa mwenye bashasha tele alipogundua anatarajia mtoto ila furaha yake ikageuka kilio takriban miezi mitatu baadae alipogundua  ujauzito wake ulikuwa umeharibika.

•Mwanavlogu huyo alifichua kuwa miezi miwili tu baada ya kupoteza ujauzito huo alifanikiwa kupata mwingine kisha akajifungua mtoto wake wa kwanza Milla Netai.

Image: INSTAGRAM// MILLY CHEBBY

Mwanavlogu mashuhuri Millicent Chebet almaarufu Milly Chebby amefunguka kuhusu kuharibika kwa ujauzito wake miaka michache iliyopita.

Akiwa kwenye mazungumzo na Diana Marua, Milly aliweka wazi kwamba alikuwa tayari kabisa kupata mtoto wake wa kwanza wakati masaibu hayo yalipomkumba.

Mke huyo wa mchekeshaji Terence Creative alisema alikuwa mwenye bashasha alipogundua  anatarajia mtoto ila furaha yake ikageuka kilio takriban miezi mitatu baadae alipogundua  ujauzito wake umeharibika.

"Nilikuwa na raha kubwa. Baada ya miezi mwili nikaanza kuspot. Nikaenda hospitali nikaambiwa mpigo wa moyo uko sawa. Nikiwa na ujauzito wa wiki 13 nilispot tena na roho yangu ikaniambia hiyo sio sawa. Hata nililia nikielekea hospitali. Nilipofika hospitalini nikaambiwa hakuna mapigo ya moyo. Ilibidi itolewe" Milly alisema.

Mwanavlogu huyo alifichua kuwa miezi miwili baada ya kupoteza ujauzito wake alifanikiwa kupata mwingine kisha akajifungua mtoto wake wa kwanza Milla Netai.

"Tulipata Milla baada ya miezi miwili. Nilipata ujauzito tena na tukampata" Alisema.

Milly alisema furaha ya kumkaribisha mtoto wake wa kwanza hata hivyo haikudumu sana kwani wiki mbili baada ya kuzaliwa aligunduliwa kuwa na ugonjwa wa tumbo.

"Nilikabiliwa na msongo wa mawazo. Niliuliza Mungu mbona nikamuomba mtoto akanipatia mwenye shida. Tumbo lake lilikuwa limefura. Hakuwa na uchungu," 

Mwanavlogu huyo alieleza kuwa masaibu hayo yalifanya aogope kupata mtoto mwingine. Hata hivyo amedai kuwa sasa y tayari kwa hatua hiyo.