Je, ni kweli Rayvanny na Lulu wana mahusiano? Diamond afichua

Muhtasari

• Katika wimbo wake wa Nawaza, Diamond anaimba kwamba huenda kuna sakata la mahaba kati ya Rayvanny na Elizabeth.

Elizabeth, Rayvanny, Diamond
Image: Instagram, Facebook

Staa wa bongo fleva Diamond Platnumz amewaacha wengi wakizungumza baada ya kuachia kipande fulani kwenye moja kati ya nyimbo za EP yake akidokeza kwamba msanii Rayvanny na muigizaji Elizabeth Lulu huenda wamewahi kuwa katika mahusiano ya kichinichini.

Katika wimbo wa Nawaza kutoka EP ya FOA, Diamond ameachia kipande kimoja chenye mistari miwili akidokeza hayo, jambo ambalo limewaacha wengi kando na kufurahia ngoma wamebaki wakichambua kipengele hicho na kudadisi kwamba huenda anajaribu kufichua skendo hiyo ya Rayvanny na Lulu.

Wimbo wa Nawaza umeibukia kuwa wimbo pendwa zaidi katika EP hiyo na ambapo sasa wengi baada ya kuusikiliza kwa mara kadhaa wamehoji ni kwa nini Diamond akatunga kipande hicho cha kuzungumzia Rayvanny na Elizabeth, ambapo haijajulikana ni Elizabeth yupi ila wengi wanahisi hap ani Elizabeth Michael Lulu.

Nawaza Vanny na Elizabeth, Clip zao zikivuja, Ndoa itaimarika eti au ndo wataivunja?” sehemu ya wimbo wa Nawaza inasema.

Wengine wanahisi kwamba ni ubunifu tu ambao Diamond alikuwa anatunga huku wengine wakisema kwamba hii ni kama njia moja ya kutumbua uhusiano haramu wa Rayvanny na Elizabeth.