Wasanii kumkumbuka E-Sir, miaka 19 tangu kifo chake

Muhtasari

• E-Sir alipatana na umauti wake katika ajali mbaya ya barabara kuu ya Nairobi kuelekea Nakuru miaka 19 iliyopita alipokuwa akirejea Nairobi kutoka hafla mjini Nakuru.

Machi 16, miaka kumi na tisa iliyopita tasnia ya muziki nchini Kenya iligubikwa na simanzi na kiza kinene baada ya taarifa za kifo cha nguli wa muziki wa wakati huo E-Sir kutangazwa.

Kifo hicho kilitokea wakiwa safarini na msanii mwenzake, Nameless kutoka Nakuru ambako walikuwa wameenda kutumbuiza.

E-sir alipoteza maisha yake ila kwa bahati nzuri Nameless aliponea na mpaka wa leo amebakia kuwa shahidi wa kuelezea jinsi matukio hayo yenye ukakasi mkubwa yalivyojiri.

Licha ya kuwa na miaka 21 wakati huo, E-Sir alikuwa ni msanii mwenye jina kubwa ndani na nje ya nchi ya mipaka ya Kenya huku akiwafurahisha mashabiki kwa vibao vyake vikali miaka ya 2000.

Jumatano hii, Machi 16 inatimia miaka 19 tangu nguli huyo wa Bomba Train aage dunia na wasanii mbalimbali wakiongozwa na aliyekuwa rafiki wake wa karibu Nameless wamekuwa wakimkumbuka kila mwaka kwa kulitembelea kaburi lake.

Mapema mwaka huu, msanii Nameless alishirikiana na msanii chipukizi Trio Mio na wengine na kuingia studioni ambapo walirekodi kibao kimoja matata kama njia moja ya kumuenzi E-Sir kwa uanzilishi wake mwema kwa muziki wa Kenya.

Kibao hicho walikibatiza kwa jina ‘Bandana ya E-Sir’ ambapo walimkumbuka msanii huyo kwa kitambaa hicho kidogo ambacho alikipenda sana kufunga kichwani mpaka kikawa kama nembo ya utambulisho wake.

Je, unahisi msanii huyo angekuwepo leo hii kungekuwqa na tofauti hasi ama chanya katika tasnia ya muziki nchini na unamkumbuka kwa ngoma ipi?