Onyi wa Real Househelps of Kawangware afunguka jinsi kufilisika kulimtenganisha na familia yake

Muhtasari

•Onyi alisema mke ambaye alikuwa anaishi naye aliondoka na kuenda kutafuta riziki kwingine baada yake kushindwa kukidhi mahitaji ya familia.

•Onyi alieleza kuwa watoto wake watano wanampenda sana na huwa wanazungumza mara kwa mara.

Mwigizaji Onyi
Mwigizaji Onyi
Image: HISANI/ TRHK YOUTUBE

Mwigizaji wa kipindi cha Real Househelps of Kawangware, Onyi amedai kwamba kufilisika kwake kulisababisha hali ya kutokuelewana kati yake na wake zake watatu.

Akiwa kwenye mahojiano na Mzuka Kibao, Onyi alifichua kwamba amekuwa pweke bila makazi tangu janga la Corona lilipokumba dunia miaka miwili iliyopita.

Onyi alisema mke ambaye alikuwa anaishi naye aliondoka na kuenda kutafuta riziki kwingine baada yake kushindwa kukidhi mahitaji ya familia.

"Mke wake alienda Kisii. Yeye ni muuguzi anafanya kazi huko. Watoto wako naye huko.. mimi sina nguvu, sina pesa hata kidogo. Hata mke wangu tunakosana naye juu ya hiyo tu," Onyi alisema.

Mwigizaji huyo alifichua kwamba yeye ni baba wa watoto watano ambao amepata na wanawake watatu tofauti.

Alieleza kuwa uhusiano wake na mama za watoto wake haujakuwa mzuri kutokana na hali ambayo ilimpata baada ya Corona kukatiza kazi zake.

"Watoto wawili nilizaa na mke wangu anayeishi Sweden, wengine wawili nilipata na mke wangu aliye Kisii, mwingine mmoja anaishi Marekani. Hatusikizani nao kabisa. Mimi sina kazi, mwanaume ni pesa," Alisema.

Licha ya kuwa na uhusiano mbaya na wake zake, Onyi hata hivyo alieleza kuwa watoto wake watano wanampenda sana na huwa wanazungumza mara kwa mara.

Alisema kuwa alikuwa anashughulikia familia yake vizuri wakati alikuwa na kazi zilizomletea kipato kizuri.