"Sijakuwa sawa kimawazo miaka 4" Mulamwah afunguka kuhusu kupambana na msongo wa mawazo

Muhtasari

•Mchekeshaji huyo ametaja takriban miaka minne ambayo imepita kuwa kipindi kibaya zaidi cha maisha yake.

•Mulamwah alidai mpenzi huyo wake wa zamani aliwahi kutoka kimapenzi na jamaa mwingine wakati bado wakiwa wanachumbiana.

Image: INSTAGRAM// MULAMWAH

Mchekeshaji David Oyando almaarufu kama Mulamwah amekiri kwamba hajawahi kuwa na amani katika kipindi kirefu zaidi cha mahusiano yake na aliyekuwa mpenzi wake, Caroline Muthoni.

Akishirikisha mashabiki wake kwenye kipindi cha maswali na majibi (Q&A) kwenye Instagram, Mulamwah alifichua amekuwa akipambana na msongo wa mawazo kwa zaidi ya miaka minne.

Mchekeshaji huyo ametaja takriban miaka minne ambayo imepita kuwa kipindi kibaya zaidi cha maisha yake.

"Sijawahi kuwa sawa kimawazo kwa zaidi ya miaka minne sasa. Sababu ziko wazi sana. Imekuwa miaka minne mbaya zaidi ya maisha yangu lakini miaka ya faida zaidi," Mulamwah alifichua kwenye Instastori zake.

Mulamwah hata hivyo alisema masaibu yake hayajamzuia kufanikiwa katika kazi zake.

Kumekuwa na hisia tofauti miongoni mwa wanamitandao baada ya msanii huyo kuibua madai kwamba Muthoni hakuwa mwaminifu katika kipindi cha mahusiano yao

Mulamwah alidai mpenzi huyo wake wa zamani aliwahi kutoka kimapenzi na jamaa mwingine wakati bado wakiwa wanachumbiana.

"Niligundua alikuwa anatoka kimapenzi na jamaa mwingine kwa zaidi ya mwaka. Kusema kweli wakati wa lockdown nilipokuwa nachoma shati kutokana na msongo wa mawazo alikuwa anaishi kwake. Hiyo ndiyo sababu tulitengana kwa mara ya kwanza," Mulamwah alijibu

Muthoni alipotembelea studio zetu mwezi Februari alisema alikuwa amempenda sana mchekeshaji huyo na hakuwahi kutoka nje ya mahusiano yao.

"Hatukuwa tunaaminiana. Sikuwahi kuwa na mahusiano ya nje. Sijui kama yeye alikuwa nayo," Muthoni alisema akiwa kwenye mahojiano na Massawe Japanni.