"Najaribu kuonyesha jinsi ninavyomhitaji!" Harmonize ajitetea kwa kutumia pesa nyingi kumtongoza Kajala

Muhtasari

•Harmonize amefichua kuwa alitumia Tsh5M kuwekewa jina la Kajala kama namba za usajili  ya Range Rovers moja katu ya mbili  aliyomnunulia.

•Harmonize amesema kuwa anampenda sana mama huyo wa binti mmoja na anajitahidi kabisa  kumuonyesha jinsi anavyomuhitaji.

Harmonize na mwigizaji Fridah Kajala Masanja
Harmonize na mwigizaji Fridah Kajala Masanja
Image: HISANI

Staa wa Bongo Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize ameendelea kuchimba ndani zaidi kwenye mifuko yake katika juhudi za kumshawishi muigizaji Frida Kajala Masanja amrudie.

Katika chapisho lake la hivi punde Harmonize amefichua kuwa alitumia Tsh5M (Ksh 250,000)  kuwekewa jina la Kajala kama namba za usajili  ya Range Rovers moja katu ya mbili  aliyomnunulia.

Harmonize alipakia video inayoonyesha akiwa ameshika vibati viwili vya nambari ya usajili na kadi ya gari.

"Hizi hapa mpenzi. Magari yote mawili tayari sasa. Tsh5M kwa jina lake tu. Nakupenda mpenzi," Harmonize aliandika juu ya video hiyo ambayo alipakia Instagram.

Wengi wamekuwa wakimkosoa mwanamuziki huyo kwa kutumia fedha nyingi kujaribu kumfurahisha Kajala ili akubali msamaha wake.

Harmonize hata hivyo amedhihirisha kuwa hajuti huku akisema anampenda sana mama huyo wa binti mmoja na anajitahidi kumuonyesha jinsi anavyomuhitaji.

"Mimi ni hustler tu na napenda mwanamke wangu. Najaribu kuonyesha jinsi ninavyohitaji arudi maishani mwangu!! Sio eti najigamba," Harmonize alisema.

Haya yanajiri huku uvumi ukiendelea kuenea kuwa wapenzi hao wawili wa zamani tayari wamerudiana. 

Tetesi kuwa wawili hao wamerudiana baada ya kutengana takriban mwaka mmoja uliopita zilianza kuenea baada ya Kajala kum-unblock mwanamuziki huyo kwenye Instagram.

Isitoshe Kajala sasa amepiga hatua zaidi ya kumfuatilia mpenzi huyo wake wa zamani kwenye mtandao huo na kuongeza zaidi tetesi za kurudiana kwao.

Hata hivyo kufikia sasa hakuna yeyote kati yao ambaye amejitokeza kuthibitisha kuwa wapo pamoja tena.