Rasmi! Kajala kuanza kazi yake Kondegang siku chache baada ya kukubali ndoa na Harmonize

"Ukiona nang'aa ujue ni kazi ya mpenzi wangu Kajala. Anaanza kazi yake rasmi leo," Harmonize alisema.

Muhtasari

•Alhamisi Kajala  anaanza rasmi kazi yake kama CEO wa timu ya usimamizi ya Konde Music Worldwide.

•Ataungana na Chopa, Mjerumani na Jose Wamipango katika timu ya usimamizi wa Harmonize na Konde Gang Music Worldwide.

mnamo siku ya kuvisha pete ya uchumba
Harmonize na Kajala mnamo siku ya kuvisha pete ya uchumba
Image: INSTAGRAM// KAJALA MASANJA

Harmonize ametangaza kuwa leo hii (Alhamisi)  mchumba wake Fridah Kajala Masanja anaanza rasmi kazi yake kama CEO wa timu ya usimamizi ya Konde Music Worldwide.

Staa huyo wa Bongo alipakia video inayomuonyesha akimsaidia Kajala kujiandaa na siku yake ya kwanza kazini.

Harmonize alionekana akimvalisha mchumba wake viatu huku wote wawili wakionekana wenye bashasha tele.

Ukiona nang'aa ujue ni kazi ya mpenzi  wangu @kajalafrida. Anaanza kazi yake rasmi leo," Harmonize aliandika chini ya video ambayo alipakia kwenye Instastori zake.

Video nyingine ilimuonyesha Kajala akiwa ameshika usakani wa moja ya Range Rovers ambazo mchumba huyo wake alimzawadi.

Haya yanajiri takriban mwezi mmoja baada ya Harmonize kumkabidhi muigizaji huyo jukumu la kuongoza timu ya mameneja wake.

Meneja wake Choppa TZ ndiye aliyetangaza habari za uteuzi wa Kajala huku akimkaribisha katika timu yao.

"Niruhusu nimkaribishe katika timu ya usimamizi mkurugenzi na meneja mpya Frida Kajala. Nimefurahi kufanya kazi na wewe shem," Choppa alitangaza kupitia Instagram.

Kajala ataungana na Chopa, Mjerumani na Jose Wamipango katika timu ya usimamizi wa Harmonize na Konde Gang Music Worldwide.

Wiki chache zilizopita mwandani wa Harmonize, Mwijaku alieleza imani yake kwa Kajala kutekeleza majukumu yake mapya.

Mwijaku alisema mama huyo wa binti mmoja ana uwezo mkubwa wa kufanya Kondegang kuwa bora zaidi.

"Kajala anaingia pale kuongeza thamani. Ana utofauti mkubwa na wanawake wengine. Anakwenda kuchora njia Kondegang kuenda kimataifa zaidi," Mwijaku alisema alipokuwa akiwahutubia waandishi wa habari.

Hatua ya Kajala kuanza kazi hiyo yake mpya inajiri siku chache tu baada ya Harmonize kumvisha pete ya uchumba.

Jambo hili lililojitokeza mwishoni mwa mwezi Juni ni dokezo kuwa wawili hao huenda wakafunga ndoa hivi karibuni.