Kundi la P Square kusambaratika tena?

Peter amesema kwamba amejiondoa kama mtangazaji wa kampuni yake ya bahati nasibu

Muhtasari

•Peter amesema kwamba amejiondoa kama mtangazaji wa kampuni yake ya bahati nasibu iitwayo ‘Zoom Lifestyle’ au ‘Zoom Up Your Life’.

•Awali Peter alikuwa ametoa ujumbe wa kujiuzulu bila maelezo ambao ulichukuliwa ndivyo sivyo na mashabiki wake.

Peter Okoye
Peter Okoye
Image: INSTAGRAM

Mwimbaji Peter Okoye ambaye ni mmoja wa kaka wawili wanaounda kundi la muziki la P Square amesema kwamba amejiondoa kama mtangazaji wa kampuni yake ya bahati nasibu iitwayo ‘Zoom Lifestyle’ au ‘Zoom Up Your Life’.

Awali alikuwa ametoa ujumbe wa kujiuzulu bila maelezo ambao ulichukuliwa ndivyo sivyo na mashabiki wake. Wengi walidhania kwamba anajiondoa kwenye kundi la P Square ambalo walifufua miezi kadhaa iliyopita.

Mwimbaji huyo kupitia ukurasa wake wa Instagram, amesema kwamba hatua yake imechochewa na matapeli ambao wamekuwa wakichukua video zake akitangaza washindi kwenye Instagram na kuzitumia kuibia watu wasio na habari mitandaoni.

Kila Jumamosi, Peter alikuwa akifanya shindano hilo la bahati nasibu na kutangaza washindi mubashara kupitia  ukurasa wake wa Instagram  ambapo aliwapigia simu moja kwa moja na kuwatumia fedha.

Anasema sasa hilo halitafanyika lakini mchezo huo utaendelea.

Alisema tiketi zote za kujiunga na mchezo zitaendelea kupatikana kwenye tovuti yao ya zoomlifestyle na wala sio kwa kutuma pesa kwenye akaunti fulani. Alifafanua kwamba, hawatumii mtandao wa Whatsapp

Okoye alizaliwa mnamo 19th ya Novemba mwaka wa 1981 pamoja na kaka yake pacha. Yeye ni Pacha wa Paul Okoye ambaye anajulikana kama Rudeboy lakini walitengana kwa muda baada ya mzozo kati yao.

Kwa sasa  yeye ndiye mliki  kampuni  bahati nasibu inayoitwa “ZOOM” na yeye ndiye Balozi wa sasa wa Tecno Mobile. Ameshinda tuzo kadhaa kama sifa kwa kazi yake.