Kinuthia afafanua kuhusu madai yake kuwa ni mjamzito

Miezi miwili iliyopiita Kinuthia alimaliza utata kuhusu jinsia yake na kuweka wazi kuwa yeye ni mwanaume.

Muhtasari

•Kinuthia alisema ni mjamzito kufuatia madai ya wanamitandao ambao wamekuwa wakidai kuwa ni mjamzito baada ya kupakia video  kwenye Tiktok.

•Takriban miezi miwili iliyopita alimaliza utata kuhusu jinsia yake na kuweka wazi kuwa yeye ni mwanaume.

Kelvin Kinuthia
Image: Mercy Mumo

Kelvin Kinuthia, tiktoker maarufu hapa nchini aliwaacha wengi na mshangao mkubwa baada ya kudai kuwa huenda ni mjamzito.

Mtambuizaji huyo ambaye utambulisho wake halisi wa kijinsia umekuwa ukihojiwa mara nyingi katika siku za nyuma aliibua madai ya ujauzito wakati wa kipindi cha Maswali na Majibu kwenye Instagram.

"Je, utapata watoto katika siku za usoni??" Shabiki wake mmoja alimuuliza Kinuthia. 

"Labda ata niko na mimba ni vile sijawaambia haya," Alijibu.

Katika mahojiano na Eve Mungai, Kinuthia alisema madai yake si ya kweli na kuweka wazi kuwa aliyasema kwa mzaha.

Alidai kuwa alichukua hatua hiyo kufuatia madai ya wanamitandao wengi ambao wamekuwa wakidai kuwa ni mjamzito baada ya kupakia video zake kwenye Tiktok.

"Nimekuwa nikerekodi video nyingi alafu watu wanaenda wanacomment hapo chini ati Kinuthia ako mimba mpaka nashangaa inatoka wapi. Unajua mtu hujibu watu na kitu wanataka kusikia. Sasa vile huyo aliuliza kama niko na mimba, si alitaka kusikia niko nayo, nikamwambia iko" Tiktoker huyo mwenye umri wa miaka 21 alieleza.

Kwa kweli uwezekano wa madai ya ujauzito wa Kinuthia kuwa kweli ni mdogo sana. Hii ni kwa sababu takriban miezi miwili iliyopita alimaliza utata kuhusu jinsia yake na kuweka wazi kuwa yeye ni mwanaume. 

Akiwa kwenye mahojiano ya awali, Kinuthia alisema kucheza uhusika wa kike kwenye video zake ni kwa ajili ya burudani na kazi tu. Alibainisha  kuwa kamwe hajawahi kukana jinsia yake ya kiume.

"Mimi ni mwanaume. Lakini nilisema siwezi wacha kufanya vitu nafanya kwa sababu watu wameniingililia ati nafanya vile na mimi ni mwanaume. Hiyo ndiyo imenifikisha mahali nipo," Kinuthia alisema katika mahojiano ya awali.

Katika mahojiano ya hivi majuzi Kinuthia alidokeza kuwa anapanga kuwa na familia yake katika siku za usoni.

Hata hivyo alibainisha kuwa hatazamii kujitosa kwenye ndoa hivi karibuni  ila baada ya takriban miaka 10.

"Si saa hii, Labda nikiwa na miaka 30 wakati tumemalizana na maisha. Saa hii ni kupiga maisha na kutafuta pesa," Alisema.

Siku za hapo nyuma mamake Kinuthia aliwahi kusema atafurahia sana wakati ambapo  mwanawe atampelekea binti mkwe.