Cebbie Koks avunja kimya baada ya dada yake Akothee kusema hatahudhuria harusi yake

Akothee alifichua kwamba hakujakuwa na uhusiano mzuri kati yake na dadake kwa takriban mwaka mmoja.

Muhtasari

•Cebbie amewashukuru wote ambao wamekuwa wakiombea ndoa yake huku mipango ya harusi yake iliyoratibiwa kufanyika Desemba ikiendelea.

•Haya yanajiri siku chache tu baada ya dada yake mkubwa Akothee kubainisha wazi kuwa hana mpango wa kuhudhuria harusi yake.

katika picha ya maktaba.
Cebbie Koks na dadake mkubwa Akothee katika picha ya maktaba.
Image: INSTAGRAM//

Dada mdogo wa Akothee, Cebbie Koks Nyasego ametoa shukran za dhati kwa watu ambao wamekuwa wakifanya juhudi za kuwasiliana naye na  kumjulia hali katika kipindi hiki ambapo ugomvi wake na dadake umekuwa gumzo mitandaoni.

Cebbie pia amewashukuru wote ambao wamekuwa wakiombea ndoa yake huku mipango ya harusi yake iliyoratibiwa kufanyika Desemba ikiendelea.

"Acheni niweke hii hapa, siwezi kujibu meseji zote. Nashukuru kwa juhudi zenu za kunifikia. Pia nakiri kwa Neema na Unyenyekevu mwingi kwamba mnaniombea kwa dhati mimi na familia yangu. Namshukuru kila anayechukua muda wake kuuombea Muungano wangu. Ndoa ni takatifu na dhaifu, siichukulii kirahisi Ahsanteni sana." alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram siku ya Jumapili asubuhi

Haya yanajiri siku chache tu baada ya dada yake mkubwa Akothee kubainisha wazi kuwa hana mpango wa kuhudhuria harusi yake.

Akothee ambaye pia anapanga kufunga pingu za maisha na mpenziwe mzungu alidokeza kuwa alilazimika kuahirisha harusi yake kwa kuwa dadake pia alikuwa na mpango wa kufunga ndoa na mchumba wake. Alidokeza kuwa ameahirisha harusi yake ambayo imesubiriwa sana hadi 2023 kutokana na mizozo ya kifamilia.

Pia alifichua kuwa hakujakuwa na uhusiano mzuri kati yake na Bi Cebbie kwa takriban mwaka mmoja sasa.

"Tuna harusi nyingine mwezi Desemba ambayo nimefurahia sana. Kitu pekee ni kwamba sikuwa nihudhurie harusi hiyo kwa sababu mimi na mdogo wangu hatujaelewana kwa takriban mwaka sasa. Nilichukua virago vyangu na kuacha uhusiano huo tarehe 31 Disemba," alisema katika video iliyosambaa mitandaoni.

Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 42  pia aliwaonya wanamitandao dhidi ya kumzungumzia dadake kwenye ukurasa wake na badala yake kuwaagiza wampatie sapoti  kwenye kurasa zake mwenyewe.

Hivi majuzi alidai kuwa ugomvi kati yake na mdogo wake umezidi kuwa mkubwa kwa kuwa mara nyingi familia yake ilikosa kuingilia kati.

Katika chapisho refu kwenye Facebook, alisema kuwa Cebbie sio dadake tu mbali alikuwa rafiki yake wa dhati hadi umaarufu ulipowatenganisha.

"Mambo yalitua kwenye meza yangu ambayo yalinivunja lakini hayakuniua🙏 ,tena hakuna mtu aliyenyoosha mkono , nilibaki kupambana peke yangu. Tena kama mkubwa wao mambo yalilazimishwa kwenye koo yangu. Nilikubali kuwa mkubwa hadi nilipopunguzwa kuwa mkeka wa mlangoni," alisema.

Mama huyo wa watoto watano alifichua kwamba alivunjika moyo zaidi wakati dadake mdogo alipodai kuwa anajifanya  katika kipindi ambacho alikuwa akipambana na msongo wa mawazo kwa takriban miezi sita.

"Niliporudi kwenye fahamu zangu, niliona ni vigumu kukubali ulikuwa mzaha, dada yangu hajawahi kunitembelea katika hospitali yoyote, si kwa njia mbaya lakini lazima alisafiri au kitu kama hicho, simlaumu,"

Alifichua kwamba mwaka jana  wakati alipokuwa amelazwa hospitalini alimwandikia dadake barua akimueleza kwa nini lazima angejitenga naye.

Hata hivyo hakutuma barua hiyo hadi  tarehe 31 kwa kuwa kila siku alitumai wangeweza kuzika uhasama wao. Pia alifichua kuwa alimblock dadake baada ya kupata ujasiri wa kutuma barua aliyokuwa amehifadhi kwa muda

"Nilisubiri dada yangu aje aseme (dada , unajua nini , samahani kwa maumivu yote niliyosababisha, tuzike yaliyopita na tujikusanye🙏) Hapana, familia iliendelea kusisitiza niwe wa kwanza kuenda kwake. Niliumia na kuumia, kwani sio mimi niliyesababisha tofauti, sio ile ninayoijua," alisema.

"Kweli, najivunia sana dada yangu, kutoka chini ya moyo wangu. Ninamtakia maisha bora zaidi, maisha yake ya baadaye yawe safi kama nyota. Nimemsamehe hadharani dada yangu, yuko na bado atabaki kuwa DAMU yangu."

Licha ya kukiri kuwa amemsamehe dada yake, aliweka wazi kuwa uhusiano kati yao hutawahi kuwa sawa tena. Pia alidokeza kwamba hatakuwa akihudhuria hafla za dadake na vilevile watu wasitarajie kumuona dadake katika hafla yake.