Wadogo zangu hawanipigi vita juu ya mali ya familia, ni wivu tu! - Akothee

Msanii huyo alizungumza alipokuwa anafafanua tofauti zilizopo baina yake na ndugu zake wadogo.

Muhtasari

• Akothee alisema kuwa ndugu wakubwa hawawezi kuwasaidia wadogo wao kisha baadaye kuwanyang'anya .

Akothee

Mwanamuziki Akothee amezungumza kuhusu ugomvi ulioko baina yake na familia yake na kuwa hakufai kuwa na utatanishi wowote.

Akothee alisema kuwa ndugu wakubwa hawawezi kuwasaidia wadogo wao kisha baadaye kuwanyang'anya .

Aliongeza kuwa yeye hawezi kuanza kubishana na wadogo wake wala kuwa na ushindani wa kifedha nao

Mkwasi huyo alieleza kuwa amekuwa akiwasaidia wadogo wake na hata kuwalipia karo ya shule walipokuwa wachanga .

"Unawezaje kushindana na mradi wako? Ni kama kushindana na wewe mwenyewe," Akothee aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Alisema kuwa familia nyingi huvunjika na ndugu kuwa na ugomvi kwa sababu ya urithi wa familia.

Akothee alisema kuwa ili familia iweze kuwa sawa, wivu haufai kuwa miongoni mwao kama njia moja ya kuzuia ugomvi wa mirathi.

Aliwaonya watu ambao hawajui ama hawajawahi jikuta katika hali kama yake wasimuingize kwenye vurugu yoyote ile.

"Kama hujui safari yangu ilivyokuwa, basi usibishane na mimi wala kutaka kushindana na mimi. Mimi ni kaa himizo kwao na wala siwezi kuwa mshindani. Hakuna kilichobadilika kwangu, ni jina tu na pesa kidogo ila bado mimi ni mtu anayewapenda zaidi na mwenye kutafuta kwa unyenyekevu," mwanamuziki huyo aliandika.

Jana Jumatano, mwanamuziki huyo alidokeza kuwa hapendi kujihusisha na familia yake kwa sababu alizotaja na kuwa alipenda kufanya mambo yake kivyake bila kuhusisha familia yake.

Akothee alisema kuwa utatanishi uliokuwa kwenye familia hiyo ulisababishwa na mkutano waliokuwa nao wa kifaimilia.

Alisema kuwa utatanishi huo uliozuka ulisababisha familia yake kutusiana na hata watu kulumbana.

Akothee alisema alikuwa na matarajio ya kuungwa mkono na familia yake kwa jambo ambalo aliwajulisha ila majibu yao ya hisia sio yale aliyokuwa akitarajia kabisa.

"Nimeshtuka sina hata maneno, mniruhusu nijiokote. Mkutano tu umefanya familia kulumbana, kutukanana na simu kupigwa kila mahali, sikuwa na ubaya, nilikuwa nawatakia mema tu," Akothee alisema.

Alisema kuwa hakuitisha familia yake msaada wowote wala kuwaita kwenye mkutano wa kuchanga pesa licha ya kuwa aliwasaidia wadogo wake.

Mwanamuziki huyo alilazimika kulinganisha tamaduni za wazungu za kuandaa hafla zao mapema ili kuzuia kuchanganyikiwa.