'Nipo huru kuolewa na nimtakaye ukiwemo mti!' Akothee athibitisha talaka na baba ya binti zake

Mwimbaji huyo amethibitisha kuwa ndoa yake na Bw Jared Okello ilivunjwa takriban mwongo mmoja uliopita.

Muhtasari

•Akothee alithibitisha kuwa ndoa yake na baba ya binti zake watatu ilivunjwa rasmi mnamo Mei  22, 2011 baada ya kesi ya talaka kuwasilishwa mwaka wa 2007.

•Aliweka wazi kwa wale wanaomwonya dhidi ya kuolewa tena kwamba yeye ni mwanamke huru bila uhusiano wowote na ndoa yake ya awali.

PICHA 1:Akothee,aliyekuwa mumewe Jared Okello na familia yao mnamo siku ya harusi yao mwaka wa 2002.. PICHA 2: Akothee na mpenzi wake wa sasa Bw Shweizer
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji mashuhuri Esther Akoth almaarufu Akothee amethibitisha talaka yake na aliyekuwa mume wake Jared Okello.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Akothee alithibitisha kuwa ndoa yake na baba ya binti zake watatu ilivunjwa rasmi mnamo Mei  22, 2011 baada ya kesi ya talaka kuwasilishwa mwaka wa 2007.

Hii ni baada ya kuwa kwenye ndoa halali  na Bw Jared kwa takriban miaka mitano.

"Hati za talaka ziliwasilishwa mnamo 2007, Amri ya Nisi (Kabisa). Kwa hivyo, ndoa hii ilivunjwa mnamo Mei 22, 2011 na Mahakama ya Juu," alisema.

Aliambatanisha ujumbe huo na picha iliyomuonyesha yeye na familia yake mnamo siku ya harusi iliyofanyika miongo miwili iliyopita.

"Harusi yetu iliyogharimu Sh2500 (Imara) Wanandoa wapya waliofunga ndoa wakionyesha malengo ya wanandoa katika kanisa la Awendo SDA mnamo tarehe 6 Julai, 2002," alisema chini ya picha hizo.

Mama huyo wa watoto watano alionyesha cheti cha talaka kutoka Mahakama ya Upeo na kubainisha kuwa ndoa yake ilivunjwa.

Aliweka wazi kwa wale wanaomwonya dhidi ya kuolewa tena kwamba yeye ni mwanamke huru bila uhusiano wowote na ndoa yake ya awali.

"Pande zote mbili ziko huru kuoa yeyote wamtakaye ikiwa ni pamoja na mti. Na maoni yako hayatashikilia maji yoyote," alisema.

Hata hivyo alitoa onyo kwa watu waliogura ndoa zao ambao hawana vyeti vya talaka dhidi ya kuolewa kwingine.

"Utakamatwa!" alionya.

Mwimbaji huyo amekuwa akikosolewa sana baada ya kudokeza mipango ya ndoa na mpenzi wake mpya, Bw Shweizer.

Akothee alifichua mahusiano yake na mzungu huyo mwezi uliopita, miezi kadhaa baada ya kutengana na Nelly Oaks.

Mwezi jana msanii huyo mwenye umri wa miaka 42 alitangaza kwamba anahisi kama maisha yake yamekamilika baada ya kukutana na Shweizer na kusema yuko tayari kutulia kwenye ndoa naye na kuwa mke mtiifu.

"Sikujua kijiji changu kingeweza kuwa Paradiso. Mfalme alikuwa akikosekana. Sasa naweza kusema maisha yangu yamekamilika na niko tayari kutulia, niko tayari kuwa mke mtiifu," Akothee alisema 

Siku za hivi majuzi amekuwa akidokeza kuhusu kufunga pingu za maisha na mzungu huyo hivi karibuni.