Mwanaume aeleza changamoto za kuishi na mwanamke asiyependa kuoga

Mwanaume huyo alisema kwamba alilazimika kuhama chumba cha malazi na kuanza kulala juu ya kochi kutokana na harufu ya kukera ya mkewe

Muhtasari

• Alisema kwamba alijaribu kumketisha mkewe chini ii kulizungumzia ila mkewe akacharuka na kumwambia kutooga kwake hakumhusu.

• Alilazimika kuhamisha malazi yake hadi sebuleni kwenye kochi kutokana na kukerwa na harufu ya mkewe.

Image: Mpasho

Hakuna kitu kinachochukiza haswa wanandoa kama kuishi pamoja na mtu ambaye hana urafiki na maji – kwa maana kwamba hapendi kuoga kabisa mpaka ashrutishwe kufanya hivyo!

Mwanaume mmoja amefichua kuwa aligundua mpenzi wake huoga mara moja kila baada ya wiki mbili walipohamia pamoja.

Mpenzi huyo wa miaka mitatu alisimulia kwamba anampenda mpenzi wake, lakini kukataa kwake kuoga kulimlazimisha kuhama chumba cha kulala na kufanya kochi moja la sebuleni kuwa malazi yake.

Kulingana na jarida la The Sun, mwanaume huyo alielezea Reedit kuwa kabla ya kuamua kuishi pamoja, hakuwa amegundua mpenzi wake alikuwa ni adui mkubwa wa maji.

“Ninampenda, lakini sikujua nilichokuwa nikiingia. Haogi mara kwa mara. Hata kidogo. Yeye huoga mara moja kila baada ya wiki. Kabla hatujahamia pamoja sikuona harufu yoyote MBAYA. Mara kwa mara alikuwa na harufu ambayo ni ya kibinadamu. Nadhani angeoga mara kwa mara kabla ya kuniona,” mwanaume huyo alinukuliwa.

Mwanamume huyo alisema kwamba baada ya miezi michache, alihisi kulazimishwa kuingilia kati, kwani hakuweza kulala kitanda kimoja na yeye.

"Baada ya miezi michache ya kujaribu kuishi nayo, nilichoka. Nilikuwa nikilala kwenye kochi kwa sababu harufu ilikuwa mbaya sana. Niliketi naye chini na kujaribu kufanya mazungumzo mazito kuhusu hilo," alisema.

Aidha alieleza kwa masikitiko kwamba hata baada ya kujaribu mazungumzo hayo naye kwa njia ya ukarimu, mpenzi wake alimcharukia kwa maneno ya kila rangi huku akimwambia kwamba kutooga kwake hakumhusu ndewe wala sikio.