Video ya mama asiye na mikono akimchezesha mtoto yapendeza wanamitandao

Mama huyo asiye na mikono alitumia miguu yake kumchezesha mtoto wake kwenye kochi.

Muhtasari

• Watu wengi walimtaja mama huyu kama mama bora zaidi duniani.

Image: Tiktok// gabymolinads

Watumizi wa mitandao walipata kufurahia video ya mwanamke asiye na mikono aliyekuwa akimwinua mwanawe mchanga kutumia miguu yake.

Kwa mapenzi mengi mama huyo anaonekana kwenye video akimwinua mtoto huyo kwa umakini na uangalifu mwingi hadi kwenye kochi na kumpakata kwa ucheshi mwingi. 

Video iliyotazamwa na zaidi ya watu laki 300 ilipata umaarufu zaidi  kutokana na hali ya mama yule alivyokuwa anajilaza kwenye kochi na kumbusu mtoto aliyetabasamu na kufurahia zaidi.

Mama huyo wa  kuigwa alionyesha kutumia kipaji cha kipekee alipomweka kwa utaratibu mtoto huyo kwenye mapaja yake. Jinsi alivyofanya ujuzi huo uliwashangaza Wanatiktok.

Wanamitandao walimpongeza na kumwombea maisha yenye afya njema na maisha marefu kumtunza na kumtimizia mahitaji mwanawe hadi aweze kujisimamia na pengine kumsaidia katika siku zake za usoni.

Wengi wa watazamaji wakituma jumbe zao kwa lugha  mbali mbali duniani walimtaja mwanamke huyo kama mama bora zaidi duniani kwa kumdekeza mtoto huyo licha ya umbile lake.

''Mungu akubariki, Tafadhali usije ukalalama wala kufa moyo'' alisema Lusikegrc kwa kumtakia mema.

"Alhamdulillah, daima nitashukuru kwa chochote nilicho nacho." Alisema Faiza.