Mrembo azirai katika jaribio la kusakata densi kwa saa 130 kuweka rekodi ya dunia

Taarifa zilidai kwamba binti huyo alikuwa amefanikiwa kucheza densi kwa saa 24 kabla ya kulemewa na kuanguka jukwaani akiwa anatiririsha shindano hilo moja kwa moja Instagram yake.

Muhtasari

• Wasaidizi wake waliojitolea na watazamaji wengine kwenye hafla hiyo walianza kuchukua hatua mara moja.

Image: screengrab

Msichana mmoja katika taifa la Nigeria ameripotiwa kuanguka na kuzirai baada ya kujaribu kusakata densi kwa saa 130 bila kukoma ili kuweka rekodi ya dunia katika kitabu cha rekodi cha Guiness.

Kulingana na blogu za nchini humo, siku chache zilizopita, alishiriki kwenye Instagram mpango wake wa kuweka rekodi mpya ya muda mrefu zaidi wa kucheza dansi kwa kushiriki katika dansi za kigeni kwa masaa 130.

Cha kusikitisha ni kwamba, video iliyoibuka kwenye mitandao ya kijamii ilinasa wakati wa kutatanisha wakati mwanadada huyo alipozidiwa na uchovu jukwaani, kufuatia saa za kucheza dansi bila kuchoka.

Wasaidizi wake waliojitolea na watazamaji wengine kwenye hafla hiyo walianza kuchukua hatua mara moja, wakimkimbilia kumsaidia walipomwona akipoteza usawa wake bila kutarajia na kuanguka jukwaani.

Katika taarifa zinazofungamana na hizo, jamaa mmoja naye aliripotiwa kupoteza uwezo wake wa kuona baada ya kujaribu kulia kwa Zaidi ya saa 100 bila kukoma ii kuweka rekodi ya Guiness pia.

Katika mahojiano ya hivi majuzi na BBC News, jamaa huyo raia wa Cameroon anayeishi Nigeria alifichua kwamba alipofuka kwa muda kwa takriban dakika 45 alipokuwa kwenye mbio za kuweka rekodi mpya ya dunia.

Danny alisema kuwa kutokana na hilo alilazimika kupunguza kilio chake.

"Ilinibidi kupanga upya mikakati na kupunguza kilio changu," alisema.

Alifichua kwamba jaribio hilo hatari pia lilimuacha akikabiliana na maumivu ya kichwa, macho yenye uvimbe, na uso uliofura.

Daniel alianza safari ya kulia kwa saa mia moja bila kukoma mapema wiki jana akiwa na matumaini ya kuweka rekodi mpya ya dunia.