"Maisha hayana raha, sitaki kuwa hapa!" Nazizi azungumzia maisha bila mwanawe aliyefariki

Nazizi amekiri kuwa bado ana uchungu na machozi huku kumbukumbu za mwanaye zikiendelea kumuandama.

Muhtasari

•Nazizi bado hajaweza kukabiliana na kifo cha mwanawe wa miaka mitatu, Jazeel ambaye aliaga dunia mwishoni mwa mwaka jana.

•Nazizi aliendelea kuongelea jinsi maisha yamekuwa magumu baada ya mtoto huyo mdogo ambaye pia alikuwa ni sahibu yake kufariki.

Image: INSTAGRAM// NAZIZI

Mwimbaji mkongwe wa Kenya Nazizi Hirji bado hajaweza kukabiliana na kifo cha mwanawe wa miaka mitatu, Jazeel Adams ambaye aliaga dunia mwishoni mwa mwaka jana.

Jazeel alifariki siku ya Krismasi mwaka jana kufuatia ajali mbaya iliyotokea katika hoteli ambayo Nazizi na familia yake walikuwa wakiishi wakati wa ziara yao nchini Tanzania. Mwili wa mtoto huyo baadaye ulisafirishwa hadi Kenya ambako alizikwa.

Takriban miezi minne baadaye, msanii huyo wa zamani wa bendi ya Necessary Noize amekiri kuwa bado ana uchungu na machozi huku kumbukumbu za mwanaye zikiendelea kumuandama.

Siku ya Jumatano, alishiriki video ya chumba chake kilichoonekana bila mtu na akafunguka kuhusu wakati mzuri ambao alikuwa akishiriki na marehemu mwanawe jioni.

"Wakati mgumu zaidi wa siku kwangu mbali na kuamka, huanza saa kumi na mbili jioni hadi naenda kulala, huu ni wakati ambao mimi na JAZ tulikuwa tukikumbatiana na kutazama Paw Patrol, kutunza ngozi zetu, kula pamoja, kucheza na. kuwa pamoja chumbani kwetu,” Nazizi aliandika kwenye video hiyo aliyoichapisha kwenye Instagram.

Mwanamuziki huyo aliendelea kuongelea jinsi maisha yamekuwa magumu baada ya mtoto huyo mdogo ambaye pia alikuwa ni sahibu yake kufariki.

"Ninacho sasa ni kumbukumbu na maumivu na machozi na nilitamani kwamba baada ya miezi 4 itakuwa bora lakini sivyo, ni ngumu! Maisha ni magumu na sitaki kuwa hapa bila mtoto wangu, lakini niko na hiyo inanihuzunisha sana, "alisema.

Aliongeza, "Najua kila mtu ananingoja niwe sawa tena, lakini sidhani kama siku hiyo inakuja.”

 Mwimbaji huyo mzaliwa wa Pwani pia alizungumzia njia ya kuelekea nyumbani kwao ambayo mtoto wake aliipenda na jinsi inavyomkumbusha juu yake.

"Siwezi kuamini hatawahi kuendesha gari lake kwenye njia hii tena. Mbona bado nipo hapa? Hakuna cha maana kwangu, hakuna,” alisema.

Nazizi Harji na mumewe Tanaka walitangaza kifo cha mtoto wao mnamo Desemba 27, 2023.

"Ni kwa huzuni kubwa na huzuni kuu kwamba tunathibitisha kifo cha Jazeel, mtoto mpendwa wa Nazizi Hirji Siku ya Krismasi, Desemba 25, 2023, nchini Tanzania. Tulipoteza roho hii mchanga katika ajali mbaya katika hoteli ambayo familia hiyo ilikuwa ikiishi. Alizikwa mapema leo jijini Nairobi, kwa mujibu wa dini yake,” ilisomeka sehemu ya taarifa.

Wakati huo, aliwaomba wananchi kwa ujumla na vyombo vya habari kuwapa nafasi yeye na familia yao huku wakiomboleza kifo cha mtoto wake.

"Katika nyakati hizi za giza, nuru ya maisha ya mtoto - katika kutokuwa na hatia na furaha - bila shaka ni bora zaidi. Utupu ulioachwa na hasara hauwezi kupimika, na maumivu hayawezi kuvumiliwa.

"Kwa heshima ya mwanawe, Nazizi anahimiza vyombo vya habari, mashabiki, na umma kushikilia utakatifu wa familia na thamani ya maisha kwa kuendeleza muda wa faragha na heshima wanapopitia huzuni hii isiyoelezeka," Nazizi aliomba.