Akothee hatimaye afichua chanzo halisi cha utajiri wa mumewe, Denis Shweizer

Mwimbaji huyo aliwakosoa Wakenya kwa kutaka kuhusishwa kwa mambo yasiyowahusu.

Muhtasari

•Akothee alibainisha kuwa baadhi ya Wakenya wenye wivu walidai kuwa kuna mambo ya kutiliwa shaka kumhusu mumewe.

•Mwimbaji huyo aliwakosoa Wakenya akidokeza kwamba wengi wao wanapenda kuhusishwa kwa yasiyowahusu.

Akothee na mume wake Denis Shweizer
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwanamuziki na mjasiriamali mashuhuri Esther Akoth almaarufu Akothee amewakashifu Wakenya ambao wamekuwa wakitilia shaka kazi na uhalali wa mumewe, Bw Denis Shweizer almaarufu Omosh.

Akizungumza wakati wa kipindi cha moja kwa moja kwenye Instagram wikendi, mwimbaji huyo alibainisha kuwa baadhi ya Wakenya wenye wivu walidai kuwa kuna mambo ya kutiliwa shaka kumhusu mumewe.

Akothee hata hivyo alidokeza kuwa mumewe ni mkulima ambaye amejikita zaidi katika ukulima wa biashara.

"Watu wengi walikuwa wakisema huyu jamaa haonekani kuwa kweli. Walikuwa wakisema, huyu jamaa anaonekana mwenye shaka. Kwani hawakukuona tangu Septemba? Ulikuwa unazunguka hapa. Walipokuona shambani walisema, huyu jamaa ni maskini. Kwa sababu walikuona shambani. Hawajawahi kuona mzungu huko Rongo?" alilalamika.

Wakati huo, Bw Shweizer mwenyewe aliweka wazi kwamba anamiliki mashamba ambapo anafanya kilimo chake.

"Hawajui kwamba niko na mashamba," alisema.

Akothee alifichua kwamba mazao mengi ya kazi ya ukulima wa mumewe huuzwa nje ya nchi huku akibainisha kwamba matajiri wengi katika nchi ya kuzaliwa ya Shweizer, Uswizi ni wakulima.

"Kwa kweli tunasafirisha chakula Ulaya. Waliniambia kuhusu Uholanzi, ni shamba namba moja la maua ambalo nadhani. Na kwa kweli, nchini Uswisi watu matajiri zaidi ni wakulima," alisema mwimbaji huyo.

Mama huyo wa watoto watano aliwakosoa Wakenya akidokeza kwamba wengi wao wanapenda kuhusishwa kwa yasiyowahusu.

Mwimbaji Akothee na mchumba wake Dennis Shweizer almaarufu Mister Omosh walifunga pingu za maisha katika harusi ya kifahari iliyofanyika Windsor Golf Hotel & Country Club, Nairobi mnamo Aprili 10, 2023. Harusi hiyo yake ya pili ilipambwa na wanafamilia, marafiki wa karibu, wasanii na wanasiasa mashuhuri nchini. Jumla ya watu wasiopungua 300 walialikwa kwenye hafla hiyo ya kufana.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 amekuwa gumzo kuu kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii tangu harusi hiyo kufanyika mnamo Aprili 10 huku wengi wakionekana kumuangazia zaidi mume wake Denis Shweizer. Wakenya wengi wamekuwa na shauku kubwa ya kutaka kujua mzungu huyu asiyeeleweka ni nani, anafanya kazi gani na jinsi alivyokuja kukutana na mama huyo wa watoto watano