"Tusiforce issues!" Akothee azungumza kuhusu kufeli kwa ndoa yake na Shweizer

Mwimbaji huyo alisema iwapo hilo litatokea, basi itakuwa ni talaka yake ya pili kuwahi kutokea.

Muhtasari

•Akothee amedokeza kwamba ikiwa ndoa na Bw Denis Shweizer itakosa kufaulu, basi hatakuwa na budi ila kujiondoa.

•Alibainisha kwamba aliwahi kuolewa rasmi tena mara moja tu na baba wa binti zake watatu wakubwa, Bw Jared Okello takriban miongo miwili iliyopita.

Akothee wakati wa harusi yake na Bw Shweizer, Akothee wakati wa harusi yake na Bw Jared.
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Takriban wiki mbili tu baada ya harusi yake kubwa, mwanamuziki Esther Akoth almaarufu Akothee amedokeza kwamba ikiwa ndoa na Bw Denis Shweizer itakosa kufaulu, basi hatakuwa na budi ila kujiondoa.

Akizungumza siku ya Jumatatu kupitia ukurasa wake wa Instagram, mama huyo wa watoto watano aliweka wazi kuwa iwapo hilo litatokea, basi itakuwa ni talaka yake ya pili kuwahi kutokea.

‘’Nimechukua talaka mara moja tu, labda kama hii haitafanya kazi itakuwa ya yangu ya pili. Tusiforce issues msee. Lakini si maisha,” alisema.

Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 43 alibainisha kwamba aliwahi kuolewa rasmi tena mara moja tu na baba wa binti zake watatu wakubwa, Bw Jared Okello takriban miongo miwili iliyopita.

Akothee alikuwa akilinganisha tofauti kati ya harusi zake mbili ambapo alionyesha picha tofauti za matukio hayo mawili.

"Katika miaka 21, mengi yanaweza kutokea. Bibi arusi mmoja, bwana harusi wawili tofauti. Bibi arusi tabasamu sasa,” aliandika chini ya picha hizo.

Kwa kuangalia tu, mtu anaweza kutambua tofauti kubwa sana katika picha hizo mbili ambazo alichapisha. Mama huyo wa watoto watano alionekana asiye na raha na aliyechoshwa sana katika picha ya kwanza ya harusi yake na Bw Jared ilhali kwenye picha ya harusi yake na Shweizer, alionekana mzuri, mtulivu na uso wake uling’aa sana.

Akothee na mchumba wake Dennis Shweizer almaarufu Mister Omosh walifunga pingu za maisha katika harusi ya kifahari iliyofanyika Windsor Golf Hotel & Country Club, jijini Nairobi mnamo Aprili 10.

Harusi ya mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 ilipambwa na wanafamilia, marafiki wa karibu, wasanii maarufu na wanasiasa mashuhuri nchini. Jumla ya watu wasiopungua mia tatu walikuwa wamealikwa kwenye hafla hiyo ya kukata na shoka. Ilikuwa ni harusi ya Akothee  ya pili kwani alifunga ndoa kwa mara ya kwanza na baba ya binti zake watatu, Bw Jared Okello zaidi ya miongo miwili iliyopita. 

Hapo awali, msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 aliwahi kufichua harusi yake na Bw Jared iligharimu shilingi  2,500 pekee.

Hivi majuzi, aliweka wazi kwamba ndoa yake na Shweizer  ni ya pili kwa kuwa mahusiano yake mengi ya awali hayakufikia ndoa rasmi.

Akothee aliwataka mashabiki wake kutoamini tetesi nyingi zisizo na msingi wanazoona kwenye mtandao ya kijamii.

Kwa wafuasi wangu wapya, msiingie kwenye mtego wa watu wenye wivu. Nimeolewa mara moja tu na mahusiano ambayo hayakuweza kufika kwenye ndoa 🤣🤣🤣🤣,hii ni ndoa yangu ya pili," alisema kwenye Instagram.

Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 43 alitaja madai mengi kuhusu yeye kuolewa mara kadhaa kuwa uwongo.