Cebbie Koks azungumzia ndoa zilizofeli za dada yake Akothee huku mzozo wao ukiendelea

Cebbie alibainisha kuwa hakuna shida na ndoa au mahusian kutofanikiwa kama vile ya dada yake.

Muhtasari

•Ugomvi kati ya dada hao haujamzuia Cebbie kumtetea mkubwa wake baada ya mwanablogu kukejeli ndoa zake zilizofeli.

•Cebbie alisema hakuna shida yoyote na mtu yeyote kuanza upya baada ya kufeli katika mahusiano ama ndoa moja.

katika picha ya maktaba.
Cebbie Koks na dadake mkubwa Akothee katika picha ya maktaba.
Image: INSTAGRAM//

Akothee na dada yake mdogo Cebbie Koks Nyasego wamekuwa wakizozana kwa muda sasa, jambo ambalo hawajaficha hadharani.

Mzozo kati ya ndugu hao wawili ulianza mwaka jana na mara kadhaa wameonekana wakitupiana cheche za maneno makali mitandaoni.

Hata hivyo, ugomvi kati ya wawili hao haujamzuia Cebbie kumtetea mkubwa wake baada ya mwanablogu kukejeli ndoa zake zilizofeli.

"Gwiji Akothee anamtambulisha "Omondi" ambaye ni mwanamume wa saba anayejitosa kwa ndoa naye. Tunamtakia heri katika ndoa yake ya saba na kusema "sisi ni nani tumhukumu?" mwanablogu aliandika kwenye Facebook.

Mwanablogu huyo aliambatanisha ujumbe wake na picha nane za Akothee na wanaume tofauti. Wanamitandao walimiminika chini ya chapisho hilo kutoa maoni tofauti na Cebbie ni miongoni mwa waliosukumwa kueleza hisia zao.

Katika jibu lake, Cebbie alibainisha kuwa dadake amekuwa na wanaume wanne pekee kati ya wale waliooneka kwenye picha zile na kueleza kuwa wengine wao walikuwa wahusika tu katika video za muziki wake.

"Sijui kuhusu mume wa saba unayemzungumzia. Lakini, hata ukiangalia picha zilezile ulizotumia, naona tu mumewe wa zamani ambaye ni baba wa wasichana wake watatu, baba ya wavulana wawaili, Nelly na huyu wa sasa. Wengine ni video vixen ambao kwa akili ya kawaida pekee hawawezi kujumuishwa," aliandika.

Cebbie ambaye anapanga kufunga pingu za maisha na mchumba wake mwishoni mwa mwaka huu  pia alibainisha kuwa hakuna tatizo lolote na ndoa au mahusiano yasiyofanikiwa kama vile ya dada yake.

Alisema hakuna shida yoyote na mtu yeyote kuanza upya baada ya kufeli katika mahusiano ama ndoa moja.

"Mwishowe, Akothee, tofauti na wanawake wengine, aliamua kuchukua jukumu la maisha yake na kukataa kupoteza matumaini ya kile anachoamini. Sio kila mtu anaweza lakini haimaanishi kuwa hatapewa nafasi,"

Haya yanajri siku chache tu baada ya Akothee kufunguka kuhusu ugomvi wake na dadake ambao ulianza mwaka jana.

Mwanamuziki huyo alisema kuwa Cebbie sio dadake tu mbali alikuwa rafiki yake wa dhati hadi umaarufu ulipowatenganisha.

Alidai kuwa ugomvi kati yake na mdogo wake umezidi kuwa mkubwa kwa kuwa mara nyingi familia yake ilikosa kuingilia kati.

"Mambo yalitua kwenye meza yangu ambayo yalinivunja lakini hayakuniua🙏 ,tena hakuna mtu aliyenyoosha mkono , nilibaki kupambana peke yangu. Tena kama mkubwa wao mambo yalilazimishwa kwenye koo yangu. Nilikubali kuwa mkubwa hadi nilipopunguzwa kuwa mkeka wa mlangoni," alisema.

Mama huyo wa watoto watano alifichua kwamba alivunjika moyo zaidi wakati dadake mdogo alipodai kuwa anajifanya  katika kipindi ambacho alikuwa akipambana na msongo wa mawazo kwa takriban miezi sita.

"Niliporudi kwenye fahamu zangu, niliona ni vigumu kukubali ulikuwa mzaha, dada yangu hajawahi kunitembelea katika hospitali yoyote, si kwa njia mbaya lakini lazima alisafiri au kitu kama hicho, simlaumu,"

Alifichua kuwa wakati alipokuwa amelazwa hospitalini alimwandikia dadake barua akimueleza kwa nini lazima angejitenga naye.

Hata hivyo hakutuma barua hiyo hadi  Desemba 31 mwaka jana kwa kuwa kila siku alitumai wangeweza kuzika uhasama wao. Alifichua alimblock baada ya kupata ujasiri wa kutuma barua aliyokuwa amehifadhi kwa muda

"Nilisubiri dada yangu aje aseme (dada , unajua nini , samahani kwa maumivu yote niliyosababisha, tuzike yaliyopita na tujikusanye🙏) Hapana, familia iliendelea kusisitiza niwe wa kwanza kuenda kwake. Niliumia na kuumia, kwani sio mimi niliyesababisha tofauti, sio ile ninayoijua," alisema.

"Kweli, najivunia sana dada yangu, kutoka chini ya moyo wangu. Ninamtakia maisha bora zaidi, maisha yake ya baadaye yawe safi kama nyota. Nimemsamehe hadharani dada yangu, yuko na bado atabaki kuwa DAMU yangu."

Licha ya kukiri kuwa amemsamehe dada yake, aliweka wazi kuwa uhusiano kati yao hutawahi kuwa sawa tena. Pia alidokeza hatakuwa akihudhuria hafla za dadake na pia hatarajii kumuona katika hafla yake.