Diamond kumkaribisha duniani mtoto wake wa tano mwaka huu

"Ni mwaka na wakati sahihi wa kuongeza mtoto mwinginge sasa," alisema.

Muhtasari

•Diamond alidokeza kuwa mwaka huu wa 2023 ndio wakati mzuri wa kuongeza mrithi mwingine wa himaya yake.

•Watu wake wa karibu wamedokeza kuwa mpenzi wake wa sasa Zuchu ndiye atakuwa mzazi mwenzake wa nne.

Image: INSTAGRAM// DIAMOND PLATNUMZ

Staa wa Bongo Naseeb Abdul Juma almaarufu Diamond Platnumz amedokeza mpango wake wa kupata mtoto wa tano mwaka huu.

Siku ya Jumanne, Diamond alidokeza kuwa mwaka huu wa 2023 ndio wakati mzuri wa kuongeza mrithi mwingine wa himaya yake.

"Ni mwaka na wakati sahihi wa kuongeza mtoto mwinginge sasa.. Amin Inshallah," alisema.

Hata hivyo hakuweka wazi mwanamke ambaye anapanga kupata mtoto naye katika taarifa yake fupi kwenye mtandao wa Instagram.

Baadhi ya watu wake wa karibu akiwemo ndugu yake Rommy Jons na mwandani wake wa Baba Levo hata hivyo wamedokeza kuwa anayedaiwa kuwa mpenzi wake wa sasa Zuhura Othman almaarufu Zuchu atakuwa mzazi mwenzake wa nne.

"Dada yangu @officialzuchu, zaa dumeeee," Baba Levo aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.

Baba Levo hata hivyo alimshauri binti huyo wa Khadija Kopa asikubali kubeba mimba ya Diamond kabla ya kuvishwa pete.

Diamond tayari ana watoto wengine wanne wanaojulikana ambao amepata na wanawake watatu tofauti. Tiffah Dangote

Alipata mtoto wake wa kwanza, Tiffah Dangote, pamoja na mwanasosholaiti wa Uganda Zari Hassan takriban miaka saba iliyopita na mwaka mmoja baadaye wakampata mtoto wao wa pili pamoja, Prince Nillan.

Hivi majuzi, bosi huyo wa WCB aliwasisimua wanafamilia wake baada ya kumtambulisha Zuchu kama mke wake wakati wa karamu ya kusherehekea siku ya kuzaliwa ya dada yake mkubwa Esma Platnumz.

Baada ya kutoa hotuba yake kwenye karamu hiyo, staa huyo alimwalika Zuchu na kumtabulisha kama mwenzake.

"Sasa mwenzangu Zuhura akasema angependa sana tukuje pamoja. Sasa mimi ni shabiki wa maagizo naomba aje awasilishe," Diamond alisema huku chumba cha sherehe kikijawa na shangwe na nderemo.

Kabla ya kuondoka jukwaani na kuchukua nafasi yake, mwimbaji huyo pia alimtaja Zuchu kama  wifi wa dada yake Esma.

"Hapo ndipo tutajua kama ana mapenzi na wifi wake," alisema.

Wahudhuriaji wa karamu hiyo walionekana kufurahishwa sana na utambulisho wa Diamond kwa Zuchu, ishara ya wazi kuwa wengi wao wameidhinisha uhusiano kati ya wawili hao na wapo tayari kushuhudia ndoa.