Diana Marua afunguka mizigo ya ujauzito ambayo amechoshwa nayo anapokaribia kujifungua

Mkewe Bahati alidokeza kuwa miguu yake imevimba na amekuwa akipata maumivu ya mgongo.

Muhtasari

•Siku ya Jumamosi, mama huyo wa watoto wawili alienda kufanyiwa masaji ya tumbo ya mwisho huku akisubiri kuzaliwa kwa bintiye.

•"Hivi karibuni binti yangu wa kifalme .. utahisi mguso wangu na busu zangu, hivi karibuni," alisema.

akiwa hospitalini tayari kujifungua mtoto wake wa tatu.
Mwanavlogu Diana Marua akiwa hospitalini tayari kujifungua mtoto wake wa tatu.
Image: INSTAGRAM// BAHATI

Mwanablogu mashuhuri Diana Marua ameendelea kudokeza kuwa tarehe yake ya kujifungua inakaribia kwa kasi.

Siku ya Jumamosi, mama huyo wa watoto wawili alienda kufanyiwa masaji ya tumbo ya mwisho huku akisubiri kuzaliwa kwa bintiye. Alipakia video iliyoonyesha mtaalamu akipapasa tumbo lake kubwa na mwili mzima.

Katika video hiyo, mke huyo wa Bahati alionekana akihangaika kutembea,  jambo ambalo alisema amechoshwa nalo. Alidokeza kuwa miguu yake imevimba na amekuwa akipata maumivu ya mgongo.

"Nataka kulia 😭😭😭😭😭 Hii ni massage yangu ya mwisho ya mtoto na hakika nitapeza vipindi hivi. Siwezi kungoja kusema kwaheri kwa matembezi ya pengwini na maumivu ya mgongo, miguu iliyovimba," aliandika chini ya video hiyo ambayo alichapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Kwa njia ya mafumbo, Rapa huyo pia alidokeza kwamba hivi karibuni sana atakuwa akijifungua mtoto wake wa  tatu.

Kwenye  instastori zake alielezea hamu yake kubwa ya kukutana na bintiye ambaye amekuwa akibeba kwa karibu miezi tisa.

"Hivi karibuni binti yangu wa kifalme .. utahisi mguso wangu na busu zangu, hivi karibuni," alisema.

Hivi majuzi Diana alilazimika kujitokeza kuweka mambo wazi baada ya tetesi nyingi kutanda mitandaoni kuwa amejifungua.

 Mke huyo wa Bahati alitumia kipindi cha moja kwa moja kwenye mtandao waInstagram  kuzika tetesi hizo ambapo alijitokeza na ujauzito wake mkubwa, ishara kuwa bado hajajifungua mtoto wake wa tatu.

Aliwataka watu kukomesha fununu kuwa aljifungua wiki kadhaa zilizopita na kusema wakati bado haujafika..

"Mnaona hadi shingo yangu imekuwa nyeusi. Bado sijajifungua, niko mjauzito bado, kwa wanamitandao na wanablogu wanaofikiria nilijifungua takriban mwezi mmoja uliopita, mkome kusambaza fununu hizo," alisema.

Aliwataka wanamitandao wapunguze wasiwasi na kuwahakikishia kuwa wakati wa kujifungua ukiwadia atawafahamisha.

Uvumi kuwa Diana tayari amejifungua ulianza kuenezwa takriban wiki moja iliyopita baada ya yeye na mumewe Bahati kupakia picha na video zake akiwa hospitalini na kudokeza yuko pale kwa ajili ya kujifungua.

Katika maelezo ya picha moja iliiyoonyesaha akiwa hospitalini, Diana alitangaza kuwa hayo yangekuwa makazi yake mapya kwa muda.

"Nyumbani mbali na nyumbani," aliandika chini ya video zilizomuonyesha akitembea kwenye korido za hospitali hiyo.