Diana Marua avunja kimya kuhusu madai ya kujifungua

Mwanavlogu huyo alijitokeza na ujauzito wake mkubwa kwenye Instagram live.

Muhtasari

•Diana aliwataka watu kusita kueneza fununu kuwa aljifungua takriban miezi miwili iliyopita kwani bado wakati haujatimia.

•"Nikijifungua mtajua tu. Mmeamini sasa? Ujauzito ndio huu, na hakuna kitu nimeweka, bado sijajifungua," alisema.

Image: INSTAGRAM// DIANA MARUA

Mwanavlogu Diana Marua amejitokeza kuweka mambo wazi baada ya tetesi nyingi kutanda mitandaoni kuwa amejifungua.

Siku ya Jumatano mke huyo wa Bahati alitumia kipindi cha moja kwa moja kwenye Instagram  kuzika tetesi hizo ambapo alijitokeza na ujauzito wake mkubwa, ishara kuwa bado hajajifungua mtoto wake wa tatu.

Aliwataka watu kusita kueneza fununu kuwa aljifungua takriban miezi miwili iliyopita kwani bado wakati haujatimia.

"Mnaona hadi shingo yangu imekuwa nyeusi. Bado sijajifungua, niko mjauzito bado, kwa wanamitandao na wanablogu wanaofikiria nilijifungua takriban mwezi mmoja uliopita, mkome kusambaza fununu hizo,"  alisema huku akionyesha ujauzito wake.

Aliwataka mashabiki wake wapunguze wasiwasi na kuwahakikishia kuwa wakati wa kujifungua ukiwadia atawafahamisha.

Rapa huyo hata hivyo hakuzungumzia tukio la hivi majuzi ambapo alidokeza kujifungua wakati alipopakia video akiwa hospitalini.

"Nikijifungua mtajua tu. Mmeamini sasa? Ujauzito ndio huu, na hakuna kitu nimeweka, bado sijajifungua," alisema.

Mke huyo wa Bahati alilazimika kujitokeza kuzungumzia suala hilo baada ya mashabiki wake kuchoka kusubiri ajifungue na kuanza kueneza fununu kuwa amejifungua kufuatia vidokezo vyake vingi.

Bahati amedokeza mara kadhaa kuwa Diana anakaribia kujifungua na hata kusema kuwa hawezi kaa mbali na nyumbani kwa hofu ya mkewe kupata uchungu wa leba na  kujifungua wakati wowote.

Alidokeza tena hivi majuzi baada ya kupakia picha ya mkewe akiwa amesimama kando ya gari la wagonjwa kisha kuandika tarehe 25 Oktoba 2022 chini yake. Diana pia amedokeza mara nyingi kuwa anakaribia kujifungua kuanzia wakati ambapo alisema kuwa ujauzito wake upo katika muhula wa mwisho.