Diana Marua alazwa katika wodi ya leba, tayari kujifungua

Bahati alitoa wito kwa Wakenya kumkumbuka mkewe katika maombi yao.

Muhtasari

•Siku ya Jumanne, mwimbaji Bahati alitangaza kuwa mkewe amelazwa katika hospitali akisubiri kujifungua.

•Pichani, Diana alikuwa ameshika tumbo lake kubwa huku uso wake akionyesha dalili za wasiwas

Wakati wa kujifungua wa mwanavlogu Diana Marua sasa umekaribia zaidi kuliko hapo awali.

Siku ya Jumanne, mwimbaji Bahati alitangaza kuwa mkewe amelazwa katika hospitali akisubiri kujifungua.

Bahati alimuomba Mungu amlinde mke wake katika hatua muhimu iliyo mbele yake.

"Malkia ameingia hospitalini katika Wodi ya Kujifungua. Mungu amtangulie," alitangaza.

Mwimbaji huyo aliambatanisha ujumbe huo na picha ya mkewe akiwa amekalia kitanda cha hospitali. Pichani, Diana alikuwa ameshika tumbo lake kubwa huku uso wake akionyesha dalili za wasiwasi.

Bahati alitoa wito kwa Wakenya kumkumbuka mkewe katika maombi yao.

Siku ya Jumatatu Diana alidokeza kwamba safari yake ya ujauzito hatimaye inakaribia kufika mwisho. 

Kupitia Instagram, Diana alifichua kuwa usiku wa kuamkia Jumatatu alikuwa amejawa na wasiwasi mwingi kuhusu safari iliyokuwa mbele yake.

"Mungu anajua jinsi nimekuwa na wasiwasi usiku mzima, kusubiri kwa muda mrefu kunakaribia mwisho. Nimejaribu kufahamu mateke na jinsi unavyosonga kwenye tumbo langu, nitazipeza," alisema.

"Ni wakati wa kukutana nawe. Siwezi kusubiri kukushika mikononi mwangu hivi karibuni."

Aidha, mwanavlogu huyo pia alimhakikishia bintiye ambaye bado hajazaliwa kuhusu upendo wake mkubwa kwake.

Wiki za hivi majuzi Diana na mumewe Bahati wamekuwa wakidokeza kuhusu kuzaliwa kwa mtoto wao wa tatu.