Bahati akiri kukosa jina la kumpa bintiye huku kuzaliwa kwake kukikaribia

Bahati alidokeza kuwa mkewe, Diana Marua atajifungua wakati wowote.

Muhtasari

• Bahati alipakia picha za kupendeza akiwa na  mkewe Diana Marua na kumwandikia bintiye ujumbe maalum.

•Diana alieleza jinsi amekuwa na hamu ya kukutana na binti yake

Bahati na Diana Marua

Mwanamuziki Kevin Kioko almaarufu Bahati amedokeza kuwa amekuwa akijitahidi kumtafutia jina mtoto anayetarajia na mke wake,Diana Marua .

Katika ukurasa wake wa Instagram, Bahati alipakia picha za kupendeza akiwa na Marua na kumwandikia bintiye ujumbe maalum.

Bahati alisema kuwa umesalia muda wa siku au masaa machache  kabla ya familia yake kumkaribisha mgeni.

Hata hivyo, Bahati ameonekana kutamaushwa na suala la kukosa kupata jina bora la kumpa binti yake huku wakati ukiendelea kudidimia.

"Kwa Binti Yangu💓... Ni Wakati, najua kuwa utakuwa hapa dakika yoyote kuanzia sasa lakini jambo la kusikitisha ni kwamba Baba na Mama yako bado hawajatafuta jina zuri kwa ajili yako Princess 🤦‍♂️🤦‍♀️," Bahati aliandika.

Wanandoa hao walipiga picha za ujauzito wa Diana zinazodhaniwa kuwa za mwisho kabla mama huyo hajajifungua.

Mke huyo wa Bahati pia alipakia picha za ujauzito wake akiwa na mumewe na kumwandikia binti yake ujumbe.

Alieleza jinsi amekuwa na hamu ya kukutana na binti yake kwa muda kuanzia wakati ambao alifahamu ni mjamzito.

Marua pia alidokeza kukutana na binti yake wakati wowote kuanzia leo na kusema jinsi safari hiyo ya miezi tisa ilivyokuwa ndefu.

"Mungu anajua jinsi nimekuwa na wasiwasi usiku mzima, Subira ya muda mrefu hatimaye unakaribia mwisho. Nimejaribu kustahimili mateke na harakati zako kwenye tumbo langu, nitazitamani . Ni wakati wa kukutana nawe, siwezi kusubiri kukubeba na kukumbatia mikononi mwangu hivi karibuni. Tunakupenda Princess ❤️," Marua alisema.

Marua pia amejiandaa vilivyo kumpokea binti yake kwa kumkaribisha yaya wake wa kitambo ili amsaidie katika ulezi huo wa hivi karibuni.