Mamake Zuchu hatimaye afunguka kuhusu ndoa yake na Diamond

"Mungu ndiye anajua kama nitapata mkwe au la," Zuchu alisema.

Muhtasari

•Bi Khadija amebainisha kuwa hajui kama wawili hao ambao wanadaiwa kuchumbiana wanapanga kufunga pingu za maisha.

•Aliweka wazi kuwa ikitokea Zuchu aolewe na bosi huyo wake, hana tatizo na wao kuwa pamoja kama mke na mume.

Khadija Kopa, Zuchu, Diamond Platnumz.
Image: HISANI

Gwiji wa muziki wa Taarab, Bi Khadija Kopa ameweka wazi kwamba hajui kama binti yake Zuchu yuko kwenye mahusiano na Diamond Platnumz.

Bi Khadija pia amebainisha kuwa hajui kama wawili hao ambao wanadaiwa kuchumbiana wanapanga kufunga pingu za maisha.

"Sijui, Mungu ndiye anajua. Hiyo ni mipango ya Mungu. Mungu ndiye anajua kama nitapata mkwe au la," alisema katika mahojiano na wanahabari.

"Mimi sijui mahusiano yake."

Wakati alipohojiwa kuhusu video za kimapenzi za binti yake na Diamond ambazo zimekuwa zikivuma kwenye mitandao ya kijamii siku za hivi majuzi, alidai kuwa hana habari kuzihusu  na hajapata nafasi ya kuzitazama.

Hata hivyo, aliweka wazi kuwa ikitokea Zuchu aolewe na bosi huyo wake, hana tatizo na wao kuwa pamoja kama mke na mume.

"Mimi sijali nini wala nini, yeyote ata mwenye amebeba mizigo kama amempenda atamuoa tu," alisema.

Pia alibainisha kuwa yuko sawa na aina ya muziki ambao binti yake anafanya akiwa katika lebo ya Diamond, WCB.

Tetesi za mahusiano kati ya Diamond na msanii wake Zuchu zimefufuliwa tena katika siku za hivi majuzi kufuatia matendo yao pamoja ambayo yamekuwa yakishirikishwa kwenye mitandao mbalimbali. Kumekuwa na video na picha kadhaa ambazo zimeibua maswali chungu nzima kuhusu uhusiano wao halisi.

Pia kumekuwa na tetesi kuwa wanapanga kufanya harusi mnamo mkesha wa mwaka mpya ambapo wameanda tamasha.

Siku chache zilizopita, meneha wa Diamond Babu Tale alitoa ombi maalum kwa wawili hao kufunga pingu za maisha mnamo siku ya kufunga mwaka huu, Disemba 31,  ambayo pia itakuwa siku ya  kuadhimisha kuzaliwa kwake.

Katika ujumbe wake, Tale alimbainishia Diamond kuwa zawadi pekee anayotamani toka kwake mnamo siku hiyo ni harusi yake na Zuchu.

"Ombilangu kwa ndugu wasanii Diamond Platnumz na Zuchu hii tarehe ni siku ya kumbukizi ya kuzaliwa kwangu, najua kijana wangu Diamond vizawadi vya magari mara nyumba ni sehemu ya kawaida sana kwako ila mimi zawadi pekee utakayo nipa na itakayo ni furahisha siku hii kwanza upige ndoa hata ya watu wanne na mashahidi kadhaa inatosha.

Pili kwenye shoo mkaniimbie kwa pamoja nyimbo yangu pendwa wakati huo mkiwa bibi na bwana harusi kisha tunafunga na kufungua mwaka kwa sura mpya," Tale aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Aliambatanisha ujumbe huo na bango la tamasha ya Diamond na Zuchu iliyoratibiwa kufanyika mnamo Desemba 31.