Meneja wa WCB afichua sababu za Diamond kuchukua 60% ya mapato ya wasanii wake

Meneja huyo alisema wasanii wamekuwa wakiondoka WCB katika jaribio la kushindana na Diamond.

Muhtasari

•Mkubwa Fella alidokeza kuwa asilimia 60 ya mapato ya msanii husalia kwenye lebo ili kulipia gharama mbalimbali.

•Meneja huyo pia alidokeza kuwa wasanii wamekuwa wakiondoka kwenye WCB katika jaribio la kushindana na Diamond.

Diamond Platnumz na meneja wa WCB Mkubwa Fella
Image: INSTAGRAM// MKUBWA FELLA

Mikataba ya WCB inaelekeza msanii kupata asilimia 40 pekee ya mapato yake yote, mmoja wa mameneja wa lebo hiyo Mkubwa Fella amethibitisha.

Katika mahojiano na Wasafi Media, Mkubwa Fella alidokeza kuwa asilimia 60 ya mapato ya msanii husalia kwenye lebo ili kulipia gharama mbalimbali.

Meneja huyo alisema pesa zinazosalia kwenye lebo hutumika kulipa mishahara na kugharamia utayarishaji na uuzaji wa muziki.

"Mi nilichungulia kuna mkataba mmoja una 40% kwa 60%. Asilimia 40  ni za msanii kutumia na ndugu zake. Asilimia 60 kuna meneja, kuna mkurugenzi lakini bado kuna hela ya kusaidia muziki wa yule msanii maanake kuna kurekodi, kuna kufanya video, kuna kurekodi, kuna promotion.. vitu vyote vinafanyika kwa mwendo huo," Mkubwa alisema.

Hivi majuzi lebo hiyo ya Diamond Platnumz imekuwa ikikosolewa sana huku ikidaiwa kuwa mikataba yake inawakandamiza wasanii.

Mkubwa Fella amewasuta wakosoaji  wa WCB na kubainisha kuwa mikataba yake ni ya haki kwa pande zote.

Meneja huyo mkongwe alidokeza kuwa wasanii wamekuwa wakiondoka kwenye WCB katika juhudi za kushindana na Diamond.

"Pigana kijana, weka muziki wako vizuri. Nawe producer kama unataka kutengeneza ngoma za Naseeb, mwambie unataka kumtengenezea ngoma. Lakini tusitake kujifanya Naseeb. Naseeb ashakuwa nembo ya taifa, napenda mtu anapoenda huko naye aende akatengeneze koo yake," Alisema.

Rayvanny ni msanii wa hivi punde kuondoka Wasafi baada ya kuwa chini ya usimamizi wa lebo hiyo kwa miaka sita.

Wakati akitangaza kuondoka kwake, staa huyo alishukuru uongozi mzima wa WCB  ukiongozwa na Diamond ambaye amekuwa mwandani wake kwa kipindi kirefu.

“Miaka 6 sasa tangu tumeanza kufanya kazi pamoja na hii timu yangu, familia yangu, WCB Wasafi. Upendo, umoja vimekuwa nguzo kubwa saba kama timu. Mengi nimejifunza lakini pia mengi tumefanikisha tukiwa pamoja.. Shukrani za dhati kwa familia yangu Wasafi lakini pia kwa ndugu yangu Diamond Platnumz kwa kunipa nafasi dunia ione kipaji change nilichobarikiwa na mwenyezi Mungu ili kufika hapa nilipofika, kusaidia familia yangu na kufanikisha mengi katika maisha yangu,” Alisema katika video aliyopakia Instagram.

Msanii huyo anaripotiwa kuondoka kwenye lebo hiyo ya Diamond ili kuangazia kukuza lebo yake ya Next Level Music .

Ripoti kutoka Bongo zilidokeza  kuwa hatua yake kuondoka WCB  ilimgharimu takriban Tsh 800 (Ksh 40.9).