"Napenda nitukanwe!" Rayvanny avunja kimya kuhusu mapokezi baridi aliyopata Marekani

Mwimbaji huyo aliweka wazi kuwa amezoea kukejeliwa.

Muhtasari

•Rayvanny alionekana akiwaburudisha mashabiki  wachache ambao hawakuonekana kufurahia tamasha hilo.

•"Kusema kweli nimezoea hilo. Wajua  Waafrika Mashariki wanapenda sana kuweka mambo mabaya," alisema.

Image: INSTAGRAM// RAYVANNY

Staa wa Bongo Raymond Shaban Mwakyusa Rayvanny amekashifu blogu moja ya Kenya kwa kuchapisha ripoti kuhusu mapokezi baridi ambayo alipata  katika ziara yake ya kimuziki jijini Houston, Marekani.

Jumapili, blogu maarufu ya udaku ilichapisha video ya tamasha la Rayvanny la Houston ambalo lilikuwa limehudhuriwa na mashabiki wachache tu. Katika video iliyochapishwa kwenye Instagram , alionekana akiwaburudisha mashabiki  wachache ambao hawakuonekana kufurahia tamasha hilo.

Akizungumza katika kipindi cha moja kwa moja kwenye Instagram, mwimbaji huyo aliweka wazi kuwa amezoea kukejeliwa.

"Kusema kweli nimezoea hilo. Wajua  Waafrika Mashariki wanapenda sana kuweka mambo mabaya," alisema.

Aliongeza, "Hata nikifanya vizuri ama nijaze uwanja hawangepost hilo!"

Staa huyo wa bongo hata hivyo alibainisha kwamba huwa anafurahia kukejeliwa kwani huwa anapata motisha wa kuweka juhudi zaidi.

"Mimi napenda nitukanwe, napenda nisemwe , napenda nichekwe. Sipendi sifa za uwongo," alisema Rayvanny.

Mwimbaji huyo alikuwa akishirikisha mashabiki wake kwenye kipindi cha moja kwa moja huku akiwa amepumzika kitandani cha hoteli moja kubwa nchini Tanzania. Mikononi mwake alikuwa ameshikilia tuzo za Afrimma ambazo alipokea siku kadhaa zilizopita katika hafla iliyofanyika katika jimbo la Dallas, nchini Marekani.

Msanii mwenzake, zuchu alishinda tuzo yake ya Afrimma kwa mara ya kwanza kabisa ambapo alikuwa anawania katika kitengo cha Best Female East Africa.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo hizo, Zuchu aliwashukuru watu wa ukanda wa Afrika Mashariki wote waliomuaminia chini ya miaka miwili tu tangu atambulishwe rasmi kwenye Sanaa ya muziki wa Bongo Fleva na lebo ya WCB Wasafi.

Pia alimsifia bosi wake Diamond Platnumz na kumtaja kama shujaa wake ambaye muda wote na siku zote atasalia katika kumbukumbu ya moyo wake.

Rayvanny ambaye ni mkurugenzi mkuu wa lebo ya Next Level Music alifurahia baada ya kushinda tuzo hiyo kwenye kitengo cha Best Male East Africa na kusema kwamba tuzo hiyo ni kwa wote waliomuaminia katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Rayvanny alisema kuwa katika maisha yake ameshinda tuzo nyingi lakini ile ya AFRIMMA ndio ilikuwa imekosekana na hivyo kuipata ni kama kumaliza mzunguko wa tuzo kwenye rafu yake.