"Niliambiwa haiwezekani kupata mimba tena" Wahu afunguka matatizo ya kupata mtoto wa tatu

Wahu alipata mtoto wa tatu miaka tisa baada ya kujifungua mtoto wa pili.

Muhtasari

•Wahu alifichua kwamba madaktari tayari walikuwa wamemfahamisha jinsi ingekuwa vigumu kwake kupata mtoto mwingine.

•Wahu alibainisha kwamba ilikuwa ndoto yake kuwa mama wa watoto watatu na akaeleza furaha yake kuona imetimia.

Image: FACEBOOK// WAHU KAGWI

Mwanamuziki mkongwe wa Kenya Wahu Kagwi amefichua kwamba tayari alikuwa akijaribu kukubaliana na hali ya kuwa mama wa watoto wawili pekee kabla ya kubarikiwa na mtoto wake wa tatu.

Akizungumza kupitia ukurasa wake wa Facebook, mama huyo wa mabinti watatu alifichua kwamba madaktari tayari walikuwa wamemfahamisha jinsi ingekuwa vigumu kwake kupata mtoto mwingine.

Alidokeza kuwa tayari alidhani haingewahi kutokea kamwe yeye kupata mimba kwa vile alikuwa amepewa taarifa kwamba hawezi kupata ujauzito bila matibabu.

"Mwezi Januari, ikiwa mtu yeyote aliniambia kwamba ningemaliza 2022 kama mama wa watoto watatu, ningesema huo ni utani wa kikatili. Waliniambia kuwa haiwezekani kupata ujauzito tena bila msaada wa matibabu. Nilikuwa najaribu kufanya amani na kuwa mama wa watoto wawili," alisema siku ya Jumatatu.

Mke huyo wa Nameless alibainisha kwamba ilikuwa ndoto yake kuwa mama wa watoto watatu na akaeleza furaha yake kuona imetimia.

"Nina kila sababu ya kushukuru. 🙏🏾Yeye hufanya vitu vyote kuwa vyema kwa wakati wake," alisema  mwanamuziki huyo.

Nameless na Wahu walimkaribisha duniani mtoto wao wa tatu mnamo Oktoba 11, 2022 na wenzi hao walijawa na furaha.

Katika taarifa yake, Wahu alisema alifurahia kubeba mtoto wake na alitazamia kwa hamu siku ambayo angekutana naye.

"Tangu nilipojua kuwa nimekubeba nakupenda. Nimependa kila teke ulizopiga na kujigeuza, ziara za daktari ambapo niliona mapigo ya moyo wako, nimependa kukuimbia, kuzungumza nawe ...," alisema.

Wahu aliendelea kusema kuwa alikuwa na wasiwasi na safari hiyo ilimuacha na hisia tofauti.

Alimshukuru Mungu kwa kujifungua vizuri na salama.

"Nimekuwa na wasiwasi, nimesali, na kuhisi mihemko mingi kwa muda wa miezi 9 iliyopita, na hapa ndio sasa... nilipokushika mikononi mwangu kwa mara ya kwanza.

Ni ngumu kuelezea wakati huu, ninachoweza kusema ni Asante, Mungu. Umetuona. #shukrani #asanteMungu #mamaShiru #mamagirls #raisinggirls." alisema.

Wahu alijifungua mtoto wake wa tatu takriban miaka tisa baada ya kujifungua mtoto wake wa pili.