Nilikaribia kulazwa hospitalini iliposemekana mwanangu amekula fare- Mama Kinuthia afunguka

Muhtasari

•Mama Kinuthia ameweka wazi kuwa anaunga mkono mtindo wa mwanawe wa kuvalia mavazi ya kiume na ya kike.

•Mwaka uliopita Kinuthia alishtumiwa kwa kutumia nauli aliyotumiwa na jamaa kununua simu na mahitaji yake mengine.

Kelvin Kinuthia
Image: Mercy Mumo

Hivi majuzi mwanavlogu maarufu  nchini Kelvin Kinuthia aliandaa karamu ya kufana kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Kinuthia aliwaalika wanafamilia wake na marafiki kadhaa kusherehekea naye huku akitimiza miaka 21.

Mama yake alikuwa mmoja wa wageni na alitumia fursa hiyo kumsherehekea mwanawe na kuzungumzia uhusiano wake naye.

"Kinuthia nakupenda sana. Mimi ni mamako. Unajua huwa tunapelekana hapa kwa hapa, ukienda chini nakuinua. Nami nikienda chini unaniinua," Mama Kinuthia alimwambia mwananawe kupitia mahojiano na Eve Mungai.

Mama huyo wa watoto watatu alifichua kuwa ana uhusiano wa karibu sana na mwanawe huyo wa mwisho.

Alipongeza hatua kubwa ambazo Kinuthia amepiga katika kazi yake ya usanii na kumtia motisha aendelee zaidi.

"Nashukuru Mungu na namwambia asante. Kama Kinuthia aliona hiyo kazi ya Tiktok na hizo vitu anafanya ndio nzuri, aendelee," Alisema.

Mama huyo aliweka wazi kuwa anaunga mkono mtindo wa mwanawe wa kuvalia mavazi ya kiume na ya kike.

Alifichua kuwa Kinuthia alianza mtindo huo wa mavazi akiwa katika darasa la sita huku akisherehekea mafanikio ambayo umemletea.

"Wakati alianza mambo ya kuvalia mavazi ya kike, mimi nilienda Gikomba nikanunua kifurushi cha nguo. Nilimwambia achague nguo zake kisha hizo zingine apeane. Ata saa hii akiniambia kuna kitu ambacho anataka nitampatia. Siogopi," Mama Kinuthia alifichua.

Mafanikio ya Kinuthia hayajakuja virahisi, kufikia alipo amewahi kukabiliana na unyanyasaji mkubwa wa kimitandao.

Mwaka uliopita alishtumiwa kwa kutumia nauli aliyotumiwa na jamaa kununua simu na mahitaji yake mengine.

Mama Kinuthia amefichua kuwa kisa hicho cha Septemba 2021 kilimuathiri sana kiasi cha kukaribia kulazwa hospitalini.

"Hiyo kitu ilifanya karibu niende nikalazwe hospitali. Hizo stori si poa. Anawezaje kuambiwa eti amekula fare. Hiyo pesa hata inaweza kuingia kwa simu. Hata niliwaita mkutano nyumbani ili kueleza," Alisema.

Hata hivyo alipata uhakika kuwa madai hayo yalikuwa ya uwongo kwa kuwa maelezo ya mshukiwa hayakuwiana na ya mwanawe.

Wakati huo huo Mama Kinuthia amewakashifu wanamitandao wenye chuki ambao wamekuwa wakielekeza maneno hasi kwa mwanawe.