Sababu kuu ya Harmonize kuyapigania sana mahusiano yake na Kajala

Konde Boy amedai kuwa muigizaji huyo anamfahamu hata zaidi ya mama yake mzazi.

Muhtasari

•Harmonize amesisitiza kuwa mchumba wake Frida Kajala Masanja anamfahamu zaidi ya mtu mwingine yeyote.

•Kati ya Machi na Mei Harmonize aliomba msamaha kwa Kajala  mara si haba na kufanya mengi katika juhudi za kurejesha mahusiano ya

mnamo siku ya kuvisha pete ya uchumba
Harmonize na Kajala mnamo siku ya kuvisha pete ya uchumba
Image: INSTAGRAM// KAJALA MASANJA

Staa wa Bongo Harmonize amesisitiza kuwa mchumba wake Frida Kajala Masanja anamfahamu zaidi ya mtu mwingine yeyote.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram Konde Boy amedai kuwa muigizaji huyo anamfahamu hata zaidi ya mama yake mzazi.

"Ananijua bora kuliko mtu yeyote, hata mama yangu katika umri huu!" Msanii huyo aliandika.

Harmonize aliambatanisha ujumbe huo na picha inayomuonyesha akibarizi na mama huyo wa binti mmoja.

"Nakupenda homie @kajalafrida," Alisema

Hii huenda ndio sababu kuu kwa nini bosi huyo wa Kondegang alitia juhudi kubwa kurejesha mahusiano yake na Kajala mapema mwaka huu.

Sio mara ya kwanza ambapo Harmonize anakiri kuwa mchumba huyo wake anamfahamu zaidi ya watu wengine wote.

Novemba mwaka jana mwanamuziki huyo alitunga wimbo 'Mtaje' maalum kwa Kajala ambao aliuachia pamoja na albamu yake 'High School'.

Wakati akifafanua kuhusu maneno ya wimbo huo, Harmonize alimtaja muigizaji huyo kama mtu ambaye alimuonyesha mapenzi zaidi na kumuelewa vizuri zaidi ya wote.

"Samahani kama nitaumiza yeyote. Kajala alinijua zaidi. Alikuwa anajua mimi ni mtu wa aina gani na napenda nini kwa wakati gani. Naamini alikuwa ananifahamu vizuri. Niamini, sitaki kuenda zaidi kueleza ilivyokuwa lakini nataka kuchukua fursa hii kama mwanaume kumuomba msamaha. Nahisi kilichofanyika ni mimi nilisababisha.Sipendezwi na kilichotokea kama mwanaume. Mimi ni mwanaume, lawama zote zije kwangu" Alisema Harmonize.

Wakati huo Konde Boy alikiri kuwa alijuta mzozo uliotokea kati yake na Kajala kuhusu binti yake huku akimsifia kama mama bora..

Aidha  aliweka wazi kuwa hakuwahi kuwa na chuki yoyote kwa Paula na kudai kuwa alimpenda kama mtoto wake tu.

"Haijalishi nini, sikufaa kureacti vile. Nahisi vibaya sana. Naona niliingiza mtu kwenye matatizo, mambo ya kupelekana kwa polisi. Nimefanya aonekane sio mama bora. Ninachoamini na najua, Kajala alikuwa anajaribu sana kwa binti yake. Alijaribu sana kumfanya bintiye bora. Naamini yeye ni mzuri" Harmonize alisema.

Kati ya mwezi Machi na Mei mwaka huu mwanamuziki huyo aliomba msamaha kwa Kajala  mara si haba na kufanya mengi katika juhudi za kurejesha mahusiano yao.

Takriban miezi miwili iliyopita hatimaye nuru ilipatikana na wawili hao wakarudiana. 

Mwishoni mwa mwezi Juni Harmonize alimvisha muigizaji huyo pete ya uchumba baada ya kukubali ombi la ndoa.