Diamond afichua mbinu maalum ya kutambua mwanamke anayempenda kwa dhati

Muhtasari

•Diamond alitumia video ya mwanamuziki wa marekani Alicia Keys akikabidhiwa mkufu wa almasi na mumewe Swizz Beat kama kielelezo.

•Diamond amesema mbinu hiyo itamsaidia kujua iwapo kweli mwanamke anampenda na si kwa sababu ya pesa zake.

Image: INSTAGRAM// DIAMOND PLATNUMZ

Bosi wa WCB Diamond Platnumz amefichua mbinu moja maalum ambayo inaweza kumsaidia kutambua mwanamke anayempenda kwa kweli.

Diamond alitumia video ya mwanamuziki wa marekani Alicia Keys akikabidhiwa mkufu wa almasi na mumewe Swizz Beat kama kielelezo cha jinsi anavyotarajia kufanyiwa na mwanamke anayempenda kwa dhati.

"Swizz Beatz anampa Alicia Keys mkufu wa almasi uliochangiwa na Nefertiti," Maelezo ya video ambayo Diamond alipakia kwenye Instastori zake yalisema.

Staa huyo wa Bongo alisema angependa sana kuona mwanamke akimfanyia kitu sawa na kile ambacho Swizz Beat alimfanyia mkewe.

Diamond alieleza kuwa kitendo kama hicho kingemsaidia kujua iwapo kweli mwanamke anampenda na si kwa sababu ya pesa zake.

"Nahitaji mwanamke wa kunisurprise hivi, hapo ndipo ninapoweza kuamini kuwa ananipenda na sio kwa sababu ya pesa zangu," Aliandika chini ya video hiyo.

Diamond ni miongoni mwa wasanii wanaofahamika kuwa kipenzi cha wanawake wengi kutoka kona zote za dunia.

Kando na umaarufu wake mkubwa, pia inaaminika kuwa yeye ni miongoni mwa wasanii tajiri zaidi barani Afrika. Utajiri na umaarufu mkubwa wa Diamond kwa kawaida huwavutia wanadada wengi.

Katika filamu ya Young, Famous & African ambayo iliachiwa takriban miezi sita iliyopita, Diamond alikiri kuwa yeye sio mwaminifu katika mahusiano.

"Ninajijua, mimi ni player!" Diamond alikiri wakati akifunguka kuhusu sifa zake katika filamu hiyo.

Kufikia sasa mwanamuziki huyo amewahi kuwa kwenye mahusiano kadhaa yakiwemo na Zari Hassan, Hamisa Mobetto, Wema Sepetu, Tanasha Donna, Jacqueline Wolper, Irene Uwoya, Jokate Mwogelo, Rehema Fabian, kati ya wengine wengi.

Siku za hivi majuzi kumekuwa na madai mengi kuwa anachumbiana na msanii wake Zuchu ila wawili hao wamekuwa wakikana kuwa kwenye mahusiano.