"Single!" Zuchu ahuzunika baada ya kutemwa na Diamond, afuta picha zake zote

Zuchu ametangaza kwamba yuko single baada ya kuvunjwa moyo na mpenzi wake.

Muhtasari

•Mtunzi huyo wa kibao 'sukari' alidokeza kwamba amevunjwa moyo na mpenziwe kutangaza kuwa sasa yuko single.

•Zuchu alichukua hatua ya kufuta picha za bosi wake Diamond ambaye inaamika kuwa amekuwa akichumbiana naye.

Zuchu na Diamond Platnumz
Image: INSTAGRAM// ZUCHU

Malkia wa Bongofleva, Zuhura Othman almaarufu Zuchu ameibua wasiwasi mkubwa juu ya hali ya mahusiano yake kufuatia chapisho lake la hivi punde kwenye mtandao wa Snapchat.

Siku ya Ijumaa, mwimbaji huyo mwenye sauti nzuri ya kumtoa nyoka pangoni alidokeza kwamba amevunjwa moyo na kutangaza kuwa sasa yuko single.

"Single.." aliandika na kuambatanisha na emoji ya moyo uliovunjika '💔'

Zuchu hata hivyo hakutoa maelezo zaidi kuhusu taarifa hiyo mpya na kuwaacha mashabiki wake wakiwaza na kukisia tu kilichofanyika.

Aidha, imebainika kuwa binti huyo wa gwiji wa taarab, Khadija Kopa pia alichukua hatua ya kufuta picha zote za bosi wake Diamond Platnumz ambaye kwa muda mrefu imekuwa ikidaiwa yuko kwenye mahusiano naye.

Haya yanajiri siku moja tu baada ya mtunzi huyo wa kibao 'Sukari' kuchapisha picha nzuri yake akiwa na bosi huyo wa WCB.

Kando ya picha hizo, alichapisha sehemu ya wimbo wake mpya  'Utaniua' na kuongeza tetesi za uhusiano mkubwa kati yao.

"Tukikosa stuli ni sunna kula kwenye mkeka. Unijue vizuri nkinuna mie ndo nadeka. Usije dhani kiburi uniache nkaja kuchekwa. Baby raha ya shughuli mkunwa awe na hekaheka," aliimba katika sehemu aliyoshiriki.

Wanafamilia wawili wa Diamond, Esma Platnumz na Romy Jons walionekana kuidhinisha ndoa yao na kumkubali Zuchu kama shemeji mpya.

Huku akitoa maoni yake chini ya chapisho hilo la Zuchu kwenye mtandao wa Instagam siku ya Ijumaa, Esma ambaye ni dada mkubwa wa Diamond alimtaja malkia huyo wa muziki wa bongofleva kama 'Bi Harusi'.

Zuchu alijibu ujumbe wa shemeji huyo wake kwa emoji za kicheko "😂😂"

Image: SNAPCHAT// ZUCHU

Binamu yake Diamond, Rommy Jons kwa upande wake aliitakia kheri ndoa yake inayotarajiwa na kipusa huyo kutoka Zanzibar.

"Na ndoa yenu ikawe na kheri Inshallah," aliandika chini ya picha ya wapenzi hao wawili ambayo alipakia kwenye ukurasa wake.

Siku chache zilizopita, Zuchu alishindwa kuficha furaha yake baada ya Diamond kumtumia ujumbe mzuri wa siku ya wapendanao.

Katika barua ambayo Zuchu ' alionyesha, Diamond alimweleza kwanini hakumtumia zawadi kemkem mnamo siku ya Valentine's kama jinsi wanaume wengine wengi ulimwenguni kote walivyowafanyia wapenzi wao.

"Kheri ya siku ya wapendanao mpenzi. Ndio, najua unadhani nimechelewa, sijachelewa kwa sababu kwetu kila siku ni siku ya wapendanao. Ndio maana sikutaka kukuletea chochote jana (Februari 14) ili ujue kwamba jana  sio siku tu, ila kwetu kila siku ni siku muhimu," ujumbe wa Diamond ulisoma.

Bosi huyo wa Wasafi aliendelea kumweleza Zuchu jinsi alivyombadilishia mtazamo wake wa siku ya Wapendanao duniani.

Pia alichukua fursa kumhakikishia binti huyo wa malkia wa mipasho, Khadija Kopa, kuhusu mahaba yake mazito kwake.

"Siku ya Valentine’s haikumaanisha chochote kwangu hapo awali. Nataka ujue kwamba nakupenda jana, leo, kesho , kila dakika na kila sekunde ya maisha yetu," 

Diamond zaidi alimuombea mpenzi huyo wake furaha isiyo na kifani na baraka za Mungu tele maishani.

"Mungu ajaze moyo wako furaha na pochi kwa pesa ili uweze kununua ardhi na Nyumba zaidi Zanzibar," aliandika.

Zuchu ambaye alishindwa kabisa kuficha furaha yake alifichua jinsi alivyowezwa na hisia na kuangua kilio cha furaha baada kupokea ujumbe huo mzuri wa mapenzi kutoka kwa anayeusisimua mtima wake.

"Nimelia kama fala. Ataniua," alisema kando ya picha ya barua ya Diamond ambayo alionyesha siku ya Jumatano.