"Wanaume wasio na aibu!" Lilian Ng'ang'a awasuta watangazaji waliomdhihaki kwa kumtema Mutua

Muhtasari

•Mtangazaji huyo alisema kabla Mutua kukubali 'kumpatia' Lilian sehemu ya hoteli alipaswa kwanza kumuuliza iwapo anammezea mate mwanaume mwingine.

• Ng'anga ameweka wazi kuwa yeye ni mmiliki mwenza wa hoteli ya A&L na ana hisa 50% pale, sawa na gavana Mutua.

Image: INSTAGRAM//GOVERNOR ALFRED MUTUA

Lilian Ng'ang'a amepuuzilia mbali madai kwamba alipatiwa sehemu ya hoteli na mume wake wa zamani gavana Alfred Mutua.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Ng'anga ameweka wazi kuwa yeye ni mmiliki mwenza wa hoteli ya A&L na ana hisa 50% pale, sawa na gavana Mutua.

Ng'ang'a amewasuta watangazaji wawili wa Iko Nini Podcast kwa kudai kuwa gavana wa Machakos alimpatia sehemu ya hoteli ya A&l kisha akakosa shukrani na kunyakuliwa na mwanaume mwingine.

"Nimekutana na kanda hii. Wanaume wasio na aibu! Hakuna mtu aliyenipa sehemu ya hoteli. Hoteli ni 50/50. Kampuni yenye ukomo. Inasikitisha sana kama nyinyi ni baba wa wasichana. Aibu kwenu!" Ng'ang'a aliandika chini ya video ya Mwafreeka akimkejeli.

Katika kanda hiyo, Mwafreeka alidai kuwa gavana Mutua alimkabidhi mke huyo wake wa zamani sehemu ya hoteli.

Mtangazaji huyo alisema kabla Mutua kukubali 'kumpatia' Lilian sehemu ya hoteli alipaswa kwanza kumuuliza iwapo anammezea mate mwanaume mwingine.