Zari ashiriki muda na babake baada ya kuolewa, ajigamba na pete yake ya ndoa

Mwanasosholaiti huyo alionekana akijivinjari na mume wake Shakib kwenye kilabu nchini Uganda.

Muhtasari

•Jumatatu, Zari alifichua kwamba alishiriki siku pamoja na baba yake mzazi ambapo alimsaidia  kazi za shambani.

•Zari pia alionyesha video nyingine ambapo wote walikuwa kwenye gari huku akionyesha pete yake ya uchumba.

Zari Hassan
Image: HISANI

Mwanasoshalaiti Zari Hassan amekuwa katika nchi yake ya asili, Uganda katika kipindi cha siku chache zilizopita.

Mama huyo watoto watano na mume wake, Shakib Cham Lutaaya ambao walifunga pingu za maisha (Nikah) hivi majuzi wamekuwa wakichapisha matukio mbalimbali ya ziara yao katika nchi hiyo jirani.

Zari alitangaza ziara hiyo wikendi kupitia ukurasa wake wa Instagram.

"Nyumbani kutamu nyumbani," aliandika kwenye picha iliyomuonyesha akiwa amesimama nje ya nyumba yake ya kifahari Uganda.

Jumatatu, alifichua kwamba alishiriki siku pamoja na baba yake mzazi ambapo alimsaidia  kazi za shambani.

Alichapisha video yake akivuna mazao shambani na kudokeza kuwa licha ya kuishi maisha ya kifahari jijini kwa miaka mingi, bado hajasahau kazi ya ukulima kama alivyofundishwa na mzazi wake miaka iliyopita.

"Baba bado anashangaa ni jinsi gani, baada ya miaka 23 ya kuishi katika majengo marefu ya Johannesburg, maisha ya Sandton kwenye barabara za haraka na njia za bunge la Pretoria hayajanibadilisha. Ni maadili baba, maadili. Nilipewa hiyo nikikua, na bado inaniishi. Nitashikilia hilo milele na siku," alisema.

Katika video zingine alizochapisha kwenye Instastori zake, alionekana akijivinjari na mume wake Shakib kwenye kilabu. Wawili hao walionekana kuwa na furaha sana huku wakicheza pamoja na marafiki wengine.

Zari pia alionyesha video nyingine ambapo wote walikuwa kwenye gari huku akionyesha pete yake ya ndoa.

"Kheri ya siku ya wafanyikazi kutoka kwa Lutaaya's," aliandika chini ya video hiyo na kuambatanisha na emoji ya pete.

Mpenzi huyo wa zamani wa Diamond na Shakib walifunga ndoa katika hafla ya faraghani ambayo ilihudhuriwa na idadi ndogo ya watu.

Katika picha na video hafla hiyo iliyofanyika chumbani ambazo zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii, wapenzi hao walionekana wamevalia Kiislamu kabisa huku wote wakiwa wameketi kwenye mkeka uliotandikwa sakafuni.

Shakib alionekana akiinama kwa goti moja na kumvisha Zari pete ya ndoa kwa furaha kabla ya wawili hao kupigana mabusu huku watu wachache waliohudhuria hafla hiyo wakiwasherehekea kwa makofi.

Vyanzo vya habari kutoka Uganda vilidai kwamba baada ya kuvishana pete katika tukio la faraghani, wawili hao ambao wamekuwa marafiki kwa zaidi ya miaka minne waliweka Nikkah yao bayana kwa wazazi wa Zari.