Mbusii azungumzia dini yake ya Rastafari, Afichua atatawazwa kuwa Kuhani Mkuu hivi karibuni

Muhtasari

•Mbusii alifichua kwamba hapo awali alikuwa mfuasi wa dini ya Kikristo ila baadae akajiunga na Rastafari.

•Mbusii alisisitiza kwamba Rastafari ni dini sawa na dini nyingine yoyote ambayo makao yake makuu ya Kenya yako katika mtaa wa Kibera.

Mtangazaji Githinji Mwangi almaarufu kama Mbusii
Mtangazaji Githinji Mwangi almaarufu kama Mbusii
Image: MBUSII

Mtangazaji wa kipindi cha Mbusii na Lion Teketeke kwenye Radio Jambo, Daniel  Githinji Mwangi almaarufu kama Mbusii amethibitisha kwamba yeye ni mwanachama halisi wa Jumuiya ya Rastafari nchini Kenya.

Akiwa kwenye mahojiano na Daniel 'Churchill' Ndambuki katika kipindi cha Churchill Show, Mbusii alifichua kwamba hapo awali alikuwa mfuasi wa dini ya Kikristo ila baadae akajiunga na Rastafari.

Mbusii alifichua kwamba amekuwa mshiriki mwaminifu wa Rastafari na hivi karibuni Jumuiya hiyo itamtawaza kama Kuhani Mkuu.

"Saa hii nishajijua vizuri. Nilikuwa Mkristo lakini hivi karibuni nitatawazwa kama Kuhani Mkuu na Jumuiya ya Rastafari ya Kenya" Mbusii alisema.

Mbusii alisisitiza kwamba Rastafari ni dini sawa na dini nyingine yoyote ambayo makao yake makuu ya Kenya yako katika mtaa wa Kibera.

"Tunatumia Bibilia ya kawaida tu. Lakini mimi niimbe, wewe uimbe,  mwingine aimbe. Nikiguswa na neno na niitafsiri nawasomea kisha tunamedi. Nikishawasomea mwingine anawasomea. Hatuna mhubiri" Mbusii alisema.

Mtangazaji huyo alifichua kwamba alipokuwa mdogo mama yake aliishi kuamini kuwa siku moja mwanawe angekuwa mhubiri na hata aliwahi kutabiriwa kuhusu suala hilo.