Juma Jux amlimbikizia Zuchu sifa kochokocho

Muhtasari

•Jux alisema kwamba Zuchu ni mwanamuziki ambaye ana uwezo maalum wa kueleza hisia mbalimbali kupitia nyimbo na kuzifanya zikae kana kwamba zinatoka moyoni mwake.

Juma Jux amlimbikizia Zuchu sifa kochokocho
Juma Jux amlimbikizia Zuchu sifa kochokocho
Image: INSTAGRAM

Huku siku inayodaiwa kuwa maalum sana kwa Zuchu ikiwadia, wasanii na watu wengi mashuhuri wameendelea kumlimbikizia sifa huyo wa muziki wa Bongo sifa kochokocho.

Juma Jux ni mmoja wa mastaa ambao wamezungumza mengi mazuri kuhusu malkia huyo kutoka Zanzibar.

Akizungumza na Wasafi Media, Jux alimtaja  Zuchu kama mwanamuziki anayejituma na kuielewa kazi yake vizuri.

Jux alisema kwamba Zuchu ni mwanamuziki ambaye ana uwezo maalum wa kueleza hisia mbalimbali kupitia nyimbo na kuzifanya zikae kana kwamba zinatoka moyoni mwake.

"Zuchu ni msanii mzuri, anaimba vizuri na anajua anachokifanya. Anamaanisha anachokiimba. Nazikiliza nyimbo zake sana. Anatoa muziki mzuri. Akiimba mapenzi anaimba mapenzi kweli, akiumia anaumia kweli, akifurahi anafurahi kweli. Yeye ni mtumbuizaji mzuri" Jux alisema.

Mpenzi huyo wa zamani wa Vanessa Mdee alijilinganisha na Zuchu huku akieleza kwamba pia yeye amekuwa akipokea sifa za kuwa na uwezo wa kueleza hisia kupitia wimbo

Jux ni mmoja wa wasanii ambao wanaunga mkono shoo kubwa ambalo Zuchu anatarajiwa kufanya jijini Dar es salaam usiku wa Valentines.

Siku ya Alhamisi bosi wa WCB, Diamond Platnumz alionekana akiongoza maandalizi ya shoo hiyo ambayo itafanyika katika ukumbi wa Milimani City.

Watu walio karibu na Zuchu wamedokeza kwamba kando na tamasha la muziki, kitu kikubwa kinachomhusu Zuchu kitafanyika usiku huo.

Kumekuwa na madai kwamba huenda usiku ule binti huyo wa Khadija Kopa akafunga pingu za maisha na bosi wake Diamond.