Karen Nyamu aahidi kugharamia matibabu ya mwanabodaboda

Muhtasari

• Karen Nyamu ametoa ahadi ya kugharamia matibabu ya mwendesha bodaboda mmoja aliyepata ajali

• Nyamu alisema kijana huyo alimuandikia ujumbe uliomgusa kwamba alipata ajali na sasa alikuwa anapitia taabu kupata msaada wa kutoa chuma ambacho kilikuwa kimewekwa kwenye mfupa wake wa mguu

KAREN NYAMU
Image: FACEBOOK

Wakili wa mjini na mwaniaji wa kiti cha useneta Nairobi, Karen Nyamu ametoa ahadi ya kugharamia matibabu ya mwendesha bodaboda mmoja aliyepata ajali na pia kumuahidi kumnunulia gari kwa biashara ya teksi.

Mwanasiasa huyo mwenye utata mwingi alimtembelea mwendesha bodaboda huyo Enock Nyanchoka katika nyumba yake ya kupanga mtaani Kawangware baada ya jamaa huyo kumwandikia ujumbe wa kuomba msaada katika ukurasa wake wa Facebook.

Nyamu alisema kijana huyo alimuandikia ujumbe uliomgusa kwamba alipata ajali na sasa alikuwa anapitia taabu kupata msaada wa kutoa chuma ambacho kilikuwa kimewekwa kwenye mfupa wake wa mguu ili kumpa udhabiti wa kukaganya chini akiendelea kupona.

Karen alimtembelea kwake Kawangware na kumuahidi kwamba Februari 11 atampeleka katika hospitali ya kimishonari ya Kijabe na kugharamia ada zote za matibabu ya kuondoa chuma hicho mguuni.

Akiandika kwenye ukurasa wake wa Facebook, Nyamu alisema kwamba Enock alimueleza kwamba alipata ajali akiwa katika mishemishe za kila siku za kutafuta unga kama mwendesha boda boda na pia akamueleza ndoto yake ya kutaka kumiliki teksi, na hapo Nyamu akatoa ahadi ya kumtimizia ndoto yake hiyo.

“Kabla apate ajali, Enock amenieleza kwamba alikuwa ni mwendesha bodaboda na ndoto yake ni kuwa na teksi. Nitatafuta rafiki zangu na wahisani wema ili tuhakikishe tunamtimizia ndoto yake ya kuwa na teksi,” aliandika Nyamu

Wakili huyo ambaye analenga kuwakilisha watu wa Nairobi katika bunge la Seneti amekuwa na utata huku visa tatanishi vikimwandama akitajwa kuwa katika mahusiano na msanii Samidoh licha ya kujua kwamba mwanamuziki huyo wa Mugithi ana mke.

Juzi picha za Nyamu akimbusu mwanamme aliyedaiwa kuwa mjumbe wa bunge la kaunti ya Nairobi zimesambazwa mitandaoni lakini baadae Nyamu alijitoa wazi na kukana madai hayo.