Harmonize na Diamond kuoneshana ubabe tarehe 4, Machi

Muhtasari

• Harmonize atangaza kutoa wimbo mpya siku ambayo Diamond anatarajiwa kuachia albamu yake ya kwanza kabisa katika safari yake ya muziki.

• Tukio hili limetajwa kuwa ni vita vya ubabe ambavyo anajaribu kumpiga aliyekuwa bosi wake na ambaye alimtoa kimuziki, Diamond Platnumz

Harmonize na Diamond
Harmonize na Diamond
Image: INSTAGRAM

Ugomvi na vita vya kibabe kati ya msanii Diamond Platnumz na Harmonize haupo karibu kabisa na kufikia mwafaka kwani wawili hao wanazidi kuchimbana mikwara kila uchao kwa maneno na vitendo pia.

Hii ni baada ya msanii Diamond kutangaza juzi kati kwamba Machi tarehe nne ataachia albamu yake mpya nay a kwanza kabisa katika safari yake ya muziki na siku chache baadae, usiku wa Februari 20, msanii Harmonize ametangaza kuwa yupo studioni akirekodi ngoma ambayo ameitaja kuwa ya mwaka na ambayo ametangaza kuiachia Machi, 4, siku ambayo Diamond anaachia EP yake.

Akiandika kwenye Instagram yake, Harmonize amefichua kwamba ngoma tayari ameipiga rekodi na anaiachia tarehe nne Machi, siku moja kabla ya tamasha lake kubwa la Afro East Carnival

“Ndio nimemaliza kurekodi ngoma yam waka. Inatoka 4/3/2022, siku moja kabla ya tamasha la Afro East Carnival na ninaomba kila mmoja ajitokeze ili tuimbe Pamoja ngoma hii ya kipekee,” aliandika Harmonize.

Tangazo hili limezua maoni kinzani kwenye mitandaoni huku baadhi wakidai ni njia ya kumpiga vita aliyekuwa bosi wake katika lebo ya WCB Wasafi, Diamond Platnumz ambaye hiyo siku ndiyo anatarajia kuzindua albamu yake mpya, baada ya kukimya kwa muda.

Ngoma hiyo ambayo Harmonize ameitaja kuwa ni ya mwaka, ni single yake ya tatu chini ya mwezi mmoja baada ya kutoa zile za Mwaka Wangu na Omoyo aliyoshirikishwa na mwanamuziki wa injili, Jane Misso.

Ikumbukwe mapema mwezi jana Harmonize alitangaza kwamba mwaka huu atakuwa anatoa ngoma kila mwezi mpaka mwaka ukamilike.

Je, unahisi kitendo cha kutangaza kuachia ngoma siku ambayo Diamond anafanya uzinduzi wa albamu yake ni sahihi ama ni vita vya kichinichini anajaribu kumpiga aliyekuwa bosi wake na ambaye alimtoa kimuziki?