"Mimi ndiye mchekeshaji bora Afrika!" Eric Omondi ajipiga kifua kufuatia madai ameishiwa na ucheshi

Muhtasari

•Eric Omondi amedai kwamba kwa sasa hakuna mchekeshaji yeyote nchini Kenya anayeweza kumpa changamoto.

•Amesema kipawa chake cha uchekeshaji kinaendelea kukua zaidi kadri miaka yake inavyosonga huku akisisitiza kuwa kamwe huwa harudii vichekesho vyake.

Eric Omondi
Eric Omondi
Image: INSTAGRAM// ERIC OMONDI

Mchekeshaji Eric Omondi amewasuta wakosoaji wanaodai ameishiwa na ucheshi na hawezi tena kuburudisha vyema kama alivyokuwa miaka ya awali.

Akiwa kwenye mahojiano na Mungai Eve, Eric alijigamba kuwa yeye ndiye mchekeshaji bora zaidi sio tu humu nchini Kenya bali pia kote bara Afrika.

Mchekeshaji huyo asiyepungukiwa na drama katika taaluma yake amedai kwamba kwa sasa hakuna mchekeshaji yeyote nchini Kenya anayeweza kumpa changamoto.

"Mimi ndiye mchekeshaji bora zaidi Afrika. Kila ninapofanya uchekeshaji, huwa naua kila mtu. Huwa naua wachekeshaji wote wa hapa nchini. Mimi ndiye mchekeshaji pekee ambaye amewahi kutumbuiza mara kumi kwa masaa mawili unusu. Siwezi kupoteza" Eric alisema.

Eric alisema kipawa chake cha uchekeshaji kinaendelea kukua zaidi kadri miaka yake inavyosonga huku akisisitiza kuwa kamwe huwa harudii vichekesho vyake.

Pia aliwasuta vikali Wakenya ambao wanafanya juhudi kuangusha wasanii baada ya kuwaona wameanza  kubobea. Hata hivyo Eric amewapa changamoto wasanii wenzake kujikakamua zaidi ili kufikia kiwango kikubwa anachojigamba kuwa.

"Hutaona wasanii wakitoka nje ya Kenya. Mpaka waamke, mpaka wachekeshaji wetu waache kufanya vichekesho ambavyo wamezoea. Watu hapa nchini ni  wacheshi sana, lakini wanarudia sana" Eric alisema.

Eric amewataka wasanii wengine kujaribu mambo tofauti na yale ambayo wamezoea ili waweze kujikuza zaidi.