"Wasafi familia yangu!" Rayvanny azungumzia tetesi za kugura lebo ya Diamond, WCB

Muhtasari

•Imekuwa ikidaiwa kuwa Rayvanny anapanga kuigura lebo hiyo inayomilikiwa na Diamond Platnumz akiwa na malengo ya kujisimamia mwenyewe.

•Amesema amekuwa akishinikizwa sana na baadhi ya watu aondoke Wasafi  kwa madai kuwa ananyonywa kimuziki.

•Amesema ana heshima kubwa kwa WCB pamoja na wakubwa wake huku akiweka wazi kuwa kwa sasa anaangazia muziki wake.

Image: HISANI

Katika kipindi cha wiki kadhaa ambacho kimepita uvumi umekuwa ukitanda kwamba mwanamuziki Raymond Shaban Mwakyusa almaarufu kama Rayvanny anakusudia kuondoka katika lebo ya WCB.

Imekuwa ikidaiwa kuwa Rayvanny anapanga kuigura lebo hiyo inayomilikiwa na Diamond Platnumz akiwa na malengo ya kujisimamia mwenyewe.

Hata hivyo, staa huyo wa Bongo amejitokeza mwenyewe na kupuuzilia mbali madai hayo huku akitaja lebo hiyo kama familia yake.

Akizungumza katika hafla ya kuzindua ubalozi wake wa PM Bets, mbabe huyo wa muziki aliisifia sana lebo ya WCB na kudhihirisha wazi kuwa wakati wake kuondoka utakapofika atapiga hatua hiyo kwa heshima kubwa.

"Wasafi wameniunga mkono sana. Ikitokea Rayvanny anatoka Wasafi, Rayvanny ataambia Wasafi kwamba anatoka. Hataambia Instagram, hataambia watu kwamba anatoka.. ikifika wakati niseme kwamba sasa nataka kufanya kazi mwenyewe, sio vita, sio ugomvi, sio mapanga. Tutakaa chini tuongee na mheshimiwa Babu Tale na Diamond niwaambie nataka kufanya moja, mbili tatu nao waniambie ninachofaa kufanya. Kwa sasa Wasafi ni kama familia yangu, ni watu ambao nafanya nao kazi" Rayvanny alisema.

Kulingana na Rayvanny, sio lazima msanii akwaruzane na lebo yake ama wakubwa wake ili ajikuze zaidi.

Mwanamuziki huyo alifichua kwamba amekuwa akishinikizwa sana na baadhi ya watu aondoke Wasafi  kwa madai kuwa ananyonywa kimuziki.

"Ikifika wakati wa Rayvanny kuwa Rayvanny  basi nitakuwa, lakini kwa sasa mimi ni Wasafi. Mini ni Wasafi for life. Naamini kwamba alokusaida amekusaidia tu. Hata uende wapi kivuli chake huwezi kukikimbia" Rayvanny alisema.

Rayvanny alisema ana heshima kubwa kwa WCB pamoja na wakubwa wake huku akiweka wazi kuwa kwa sasa anaangazia muziki wake.