Davido auza tiketi zote za tamasha lake London

Muhtasari

• Davido ametangaza kuuza tiketi zote kuelekea tamasha lake kuu la The02London litakalofanyika wikendi ya Machi 5.

Msanii DAVIDO
Msanii DAVIDO
Image: INSTAGRAM// DAVIDO

Nguli wa miziki aina ya Afro Beat Davido hatimaye amefanikiwa kuuza tiketi zote za tamasha lake kubwa linalotarajiwa kufanyika wikendi hii ya Machi 5 jijini London Uingereza.

Akitangaza kwenye ukurasa wake wa Instagram, Davido alisema kwamba hatimaye tiketi zote zimeisha baada ya watu wengi kuzinunua kwa wingi mno ili kuhudhuria tamasha hilo alilolibatiza kwa jina The02London, tamasha litakalofanyika mubashara katika ukumbi wa 02, Jijini London.

Kulingana na jinsi ambavyo tiketi hizo zilishambuliwa na wafuasi na mashabiki wake mpaka kuisha, tamasha hilo linatarajiwa kuwa kubwa Zaidi kwa sababu pia miziki ya Davido imepenyeza kwa sana sio tu  nchini Nigeria na bara Afrika bali hata Ulaya na Marekani.

Hii haitakuwa mara ya kwanza kwa msanii kutoka Afrika na haswa Nigeria kujaza ukumbi nchini Uingereza kwani mwaka wa 2012 msanii Wizkid alijaza ukumbi wa Hammersmith Apollo ambapo aliuza tiketi zote na kuangusha bonge la ‘live performance’ ambayo haitawahi kusahaulika.

Nyimbo za wasanii kutoka Nigeria zimepata umaarufu mkubwa sana nchini Uingereza kwani mwaka jana Wizkid pia alitumbuiza katika tamasha moja nchini humo ambapo aliwashangaza wengi walipoonekana kwenye video wakiimba Pamoja na yeye akitumbuiza kwenye ukumbi.

Wengi walifurahishwa na jinsi ambavyo wazungu walikuwa wanaimba ngoma za msanii huyo kwa mbwembwe tele, kuonyesha kwamba huwa wanazifuatilia na hata kutenga muda wao kuzisikiliza na kujua vile zinaimbwa.

Wasanii wa Afrika Mashariki, kazi mnayo!