Mume wangu nakupenda, usiwasikilize watakuchanganya - Shilole

Muhtasari

• Mwanamuziki kutoka Tanzania, Shilole amemhakikishia mumewe kwamba penzi lao lipo imara na kumtaka  kutosikiliza maoni ya mashabiki kuhusu mahusiano yao.

• “Mpenzi wangu nataka ujue kwamba nakupenda sana, na nakuomba usiwasikilize watu, wengi watakupotosha,” Shilole alisema.

Instagram, KWA HISANI
Instagram, KWA HISANI
Image: Shilole

Mwanamuziki kutoka Tanzania, Shilole amemhakikishia mumewe kwamba penzi lao lipo imara na kumtaka  kutosikiliza maoni ya mashabiki kuhusu mahusiano yao.

Akizungumza katika mahojiano na Efm, Shilole alisema kwamba anamkubali sana mumewe na anashukuru kwa jinsi ambavyo amejitolea kumpenda na kumtunza ikifahamika kwamba penzi lake la awali na Uchebe lilikuwa na misukosuko mingi.

“Mpenzi wangu nataka ujue kwamba nakupenda sana, na nakuomba usiwasikilize watu, wengi watakupotosha,” Shilole alisema.

Rommy ambaye ni mumewe anaonekana kuwa mchanga kiumri huku baadhi ya mashabiki wakisema kwamba amedata pale kwa sababu ya pesa ila wapenzi hao wawili wameshikilia kwamba upendo umewaunganisha na watazidi kusalia pamoja.

Shilole alikuwa akiyazungumza hayo wakati alikuwa anazindua rasmi kibao chake cha #MamaNtilie ambacho kinazidi kufanya vizuri katika chati mbalimbali za muziki huko Bongo.

Siku chache zilizopita, Mwijaku alisema kwamba angetaka sana Alikiba kumchukua Shilole kama mke wake wa pili huku baadhi ya mashabiki na washikadau wakisema kwamba huenda kauli hiyo ikasambaratisha penzi la Shilole na Rommy.

Aidha aliyekuwa mpenzi wa Shilole, Nuh Mziwanda amezidi kuonyesha kudata kwake akisema kwamba angependa sana kurudiana naye ila kwa jinsi mambo yalivyo, hili litasalia kuwa ndoto tu.