Erick aandamana jijini Nairobi nusu uchi na minyororo mwilini

Muhtasari

• Mcheshi Erick Omondi amesema kwamba vijana wamefungwa minyororo ya utumwa na umaskini tangu enzi za taifa hili kupata ukoloni.

• “Wanasiasa wamewatumia vijana kwa muda sasa, imetosha! Tunataka kulikomboa taifa letu,” Omondi aliandika.

Eric Omondi
Image: Instagram

Mcheshi Erick Omondi amewashangaza wakazi wa Nairobi baada ya kujitokeza mjini akiwa nusu uchi huku akiwa amejifunga nyororo mwilini.

Mcheshi Erick Omondi amesema kwamba vijana wamefungwa minyororo ya utumwa na umaskini tangu enzi za taifa hili kupata ukoloni.

Kupitia video aliyoipakia katika ukurasa wake wa Instagram, Omondi alionekana akiwa amejifunga nyororo kwa kile alichosema ni ishara ya matatizo ambayo vijana wamekuwa wakipitia kwa muda mrefu sasa.

Omondi alisema kwamba vijana wana uwezo wa kumchagua kiongozi ambaye atapigania haki zao na kuboresha maisha yao.

Aidha aliongeza kwamba wanasiasa wamekuwa wakiwanyanyasa na kuwatumia vijana, na sasa umewadia muda rasmi wa kujikomboa.

“Wanasiasa wamewatumia vijana kwa muda sasa, imetosha! Tunataka kulikomboa taifa letu,” Omondi aliandika.

Alishikilia kwamba anawataka Raila Odinga na William Ruto kumtafuta ili kufanya majadiliano, la sivyo hakuna atakayeingia mamlakani kati yao.

Baadhi ya wasanii kama vile Nameless walipelekea katika mitandao ya kijamii kumshukuru Omondi kwa hatua na juhudi zake za kuhakikisha vijana wanapata haki zao na kuishi maisha mazuri.

“Imefika muda lazima tumpe huyu bwana maua yake angali hai, amekuwa kakamavu na stadi katika harakati zake,” aliandika Nameless.

Hatua hii ya Omondi inajiri miezi michache tu kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika tarehe 9 mwezi Agosti.