Staa wa Reggae, Jah Cure ahukumiwa kifungo cha miaka 6 gerezani

Muhtasari

•Mnamo mwezi Oktoba mwaka jana, Jah Cure, 43, alishtakiwa kwa kosa la kumdunga  kisu promota  Nicardo 'Papa' Blake. 

•Mwanamuziki huyo aliwahi kuhudumu kifungo kingine cha miaka 8 kati ya 1999-2007. 

Jah Cure alipokuwa ametembelea studio za Radio Jambo mnamo 2019
Jah Cure alipokuwa ametembelea studio za Radio Jambo mnamo 2019
Image: MOSES MWANGI

Gwiji wa reggae,  Siccature Alcock almaarufu Jah Cure atahudumu kifungo cha miaka sita gerezani kwa jaribio la kuua bila maksudi.

Mzaliwa huyo wa Jamaica alihukumiwa kifungo hicho na mahakama moja nchini Uholanzi siku ya Jumanne.

Mnamo mwezi Oktoba mwaka jana, Jah Cure, 43, alishtakiwa kwa kosa la kumdunga  kisu promota  Nicardo 'Papa' Blake. 

Mzozo wao ulihusisha takriban shilingi 630, 000 ambazo Jah Cure alimdai promota huyo kama malipo ya tamasha alilokuwa amefanya mjini Dam Square, Uholanzi. Jah Cure alikuwa anatazama kifungo cha hadi miaka 15 gerezani.

Akijitetea mahakamani mapema mwezi huu, mwanamuziki huyo alisema alikuwa anajikinga ila mahakama ikakataa madai yake. Upande wa mashtaka ulisema alikusudia kumsababisha Blake majeraha mwilini.

Mahakama  hata hivyo haikumpata na hatia ya jaribio la mauaji na badala yake akatiwa hatiani ya kujaribu kuua bila kukusudia.

Jah Cure aliwahi kuhudumu kifungo kingine cha miaka 8 kati ya 1999-2007. Alikuwa amepatikana na makosa ya wizi wa kimabavu, umiliki haramu wa bunduki na ubakaji.