Nimebadilisha sura ya EP lazima ulimwengu ututambue - Diamond

Muhtasari

• Diamond Platnumz amesema kwamba amepandisha hadhi ya EP, na sasa muziki wa bongo utajulikana zaidi.

• Alisema kwamba msanii lazima awe mbunifu ili kutoa upinzani katika viwango vya kimataifa.


Staa wa muziki wa Bongo, Diamond Platnumz amejisifia kwa kupandisha hadhi na viwango vya EP nchini humo.

Akizungumza na wanahabari katika mahojiano baada ya hafla ya kuzindua video za nyimbo zilizopo katika EP yake, Simba alisema kwamba yeye pamoja na timu yake wametumia akili na hela nyingi ili kuhakikisha EP hiyo inapata mapokezi mazuri hata katika mataifa ya kigeni.

Hakukoma kujilimbikizia sifa kuwa msanii wa kwanza ndani ya Tanzania kufanya hafla kubwa kiasi hicho kwa ajili ya EP.

Kwa kawaida EP haina sherehe nyingi ila Diamond aliandaa hafla tatu tofauti jambo linaloonyesha kwamba ilikuwa na ukubwa wake.

Aidha alisema kwamba hakufanya hivyo kuwapa presha wasanii wenzake, bali kuhakikisha kwamba wanamuziki hao wanajituma nje ya upeo wao kuachia kazi safi na zinazokubalika.

Diamond alisema kwamba atakuwa anafanya 'media tour' yake katika mataifa ya Marekani na Uingereza ili kuendelea kuuza EP hiyo.